ZANZIBAR-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC- Organ), Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameongoza Mkutano wa Dharura wa Utatu wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi hiyo unaofanyika kwa njia ya mtandao katika Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar leo Januari 5,2025.
Viongozi wengine walioshiriki katika mkutano huo ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax ( Mb.), Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Dkt. Samwel Shelukindo pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe.
Mkutano huo umehudhuriwa na Nchi za Zambia na Malawi ambao ni wajumbe wa Utatu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama (Organ Troika).
Pamoja na masuala mengine mkutano huo umejadili na kutoa mapendekezo ya namna SADC inavyoweza kuisaidia Jamhuri ya Msumbiji kukabiliana na changamoto za kisiasa zinazoendelea nchini humo.