NA MARY GWERA
Mahakama Dar
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi kwenye maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Sheria nchini, yatakayofanyika Kitaifa mkoani Dodoma tarehe 03 Februari, 2025.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (juu na chini) akizungumza na Waandishi wa Habari leo tarehe 14 Januari, 2025 kuelekea maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria kwa mwaka 2025. Wengine katika picha ya chini ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (kushoto) na Kaimu Jaji Mfawidhi Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Sharmillah Sarwatt (kulia).
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo tarehe 14 Januari, 2025 katika ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke jijini Dar es Salaam, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema Siku hiyo muhimu itatanguliwa na Wiki ya Sheria ambapo kutakuwa na maonesho ya utoaji elimu kwa umma kuhusu Mahakama na Sheria kwa ujumla kuanzia tarehe 25 Januari hadi tarehe 01 Februari mwaka huu.
“Hafla ya Siku ya Sheria (Law Day) itafanyika kwenye Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma ambapo Mgeni Rasmi kwenye kilele cha Siku ya Sheria Nchini anatarajiwa kuwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Mhe. Prof. Juma.
Aidha, Jaji Mkuu amesema kuwa, Mgeni Rasmi wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Sheria anatarijiwa kuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere (Nyerere Square) Jijini Dodoma.
“Uzinduzi wa Wiki ya Sheria utatanguliwa na Mbio Maalumu (Fun Run) za kilomita 10 ambazo zitaambatana na matembezi ya umbali wa kilomita tano kwa wale ambao watapendelea kutembea. Katika hizo mbio maalum na matembezi ya tarehe 25 Januari 2025, tutaongozwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,” ameeleza Mhe. Prof. Juma.
Jaji Mkuu amebainisha kuwa, Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria yatafanyika katika ngazi ya Kitaifa, Kanda za Mahakama Kuu, Divisheni za Mahakama Kuu, Mikoa na Wilaya zote nchini ambapo elimu ya masuala mbalimbali ya kisheria itatolewa katika maeneo mbalimbali.
“Maadhimisho ya Wiki ya Sheria ni jukwaa maalum linaloikutanisha Mahakama na wadau wake muhimu hususani wananchi ili kutoa elimu ya shughuli zinazotolewa na Mahakama na wadau wake walio katika mnyororo wa utoaji haki,” amesema Mhe. Prof. Juma.
Sehemu ya Waandishi wa Habari na Viongozi wa Mahakama wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (chini na picha mbili juu).
Ameongeza kuwa, zoezi la utoaji elimu litahusisha Majaji, Wasajili, Naibu Wasajili, Watendaji na Mahakimu na kwamba Mahakama itashirikiana na Wadau wake muhimu kama vile Tume ya Utumishi wa Mahakama, Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Tume ya Kurekebisha Sheria, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS).
Taasisi nyingine zitakazoshiriki katika kutoa elimu ni Ofisi ya Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Chama cha Majaji Wanawake (TAWJA), Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA), Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na wadau wengine.
Aidha, Jaji Mkuu ameeleza kuwa, kwa kuzingatia kwamba maadhimisho ya Wiki ya Sheria yanafanyika siku za kazi ambapo wananchi wengi wanakuwa kwenye shughuli za utafutaji wa kipato, utoaji elimu kwa mwaka huu umelenga kuwafuata wananchi karibu zaidi na maeneo yao wanayofanyia kazi tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
“Tutatoa elimu ya masuala mbalimbali ya kisheria kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi kwa kutumia magari maalumu yatakayokuwa yanahama kutoka eneo moja kwenda eneo jingine. Tutaongeza wigo wa utoaji elimu kwenye shule za msingi, sekondari na vyuo ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi,” amebainisha Mhe. Prof. Juma.
Kadhalika, amesema kwamba ili kuhakikisha elimu inawafikia watu wengi wigo wa vipindi vya utoaji elimu kwenye vyombo vya habari kupitia luninga, redio na mitandao ya kijamii utaongezeka pia ambapo ameeleza kuwa, “Ni matumaini yetu kwamba utaratibu wa mwaka huu utatuwezesha kuwafikia wananchi wengi zaidi ambao wanahitaji kupata uelewa wa masuala mabalimbali ya kisheria.”
(Picha na Faustine Kapama, Mahakama, Dar es Salaam).
Kaulimbiu ya Wiki na Siku ya Sheria mwaka huu inasema, ‘Tanzania 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo’.
Katika kutekeleza Nguzo ya Tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama (2020/2021-2024/2025), kila mwaka Mahakama huadhimisha Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria. Siku ya Sheria huashiria mwanzo wa kuanza kwa shughuli za Mahakama kwa mwaka husika baada ya kumalizika kwa likizo ya Mahakama inayoanza kila tarehe 15 Desemba na kumalizika tarehe 31 Januari ya mwaka unaofuatia.