DAR-Rais wa Benki ya Dunia (WBG), Bw. Ajay Banga amewasili nchini kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati ujulikanao kama “Mission 300”, utakaofanyika tarehe 27 hadi 28 Januari 2025 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo unalenga kuwakutanisha Wakuu wa Nchi za Afrika na wadau muhimu wa sekta ya nishati na fedha ili kujadili namna ya upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu, na endelevu kwa watu milioni 300 barani Afrika ifikapo mwaka 2030.
Benki ya Dunia imekuwa mshirika muhimu katika kusaidia miradi ya upatikanaji wa nishati nchini na barani Afrika kwa namna mbalimbali ikiwemo kufadhili miradi ya upanuzi wa gridi ya taifa, maendeleo ya nishati mbadala, gridi ndogo na usaidizi wa sera, na kuwezesha ushiriki wa sekta binafsi katika sekta ya nishati, huku ikilenga zaidi kuzifikia jamii ambazo hazijafikiwa na huduma ya nishati.
Mbali na Rais wa Benki ya Dunia, Viongozi wengine Wakuu wa Nchi na Mashirikia waliowasili nchini hadi sasa ni Rais wa Jamhuri ya Sierra Leone, Mheshimiwa Julius Maada Bio na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina.
Poja na mambo mengine mkutano huo unatarajiwa kuridhia na kusaini Mpango Mahsusi wa Nishati Afrika (Africa Energy Compact), kusaini Awamu ya kwanza ya Mipango ya Kitaifa ya Nishati kwa kipindi cha miaka mitano 2025 – 2030 (National Energy Compacts) na kupitisha Tamko la Dar es Salaam la Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika Kuhusu Nishati (Dar es Salaam Declaration on Africa Heads of State Energy Summit) ambao utajumuisha nchi 14 za Tanzania, DRC, Ivory Coast, Burkina Faso, Chad, Liberia, Madagascar, Malawi, Mauritania, Mozambique, Niger, Nigeria, Senegal na Zambia.

Wakati huohuo kupitia Mpango wa Usambazaji Umeme vijijini (REA), takriban vijiji vyote nchini vimefikiwa na huduma ya nishati ya umeme.