NA GODFREY NNKO
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amesema,katika kipindi cha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM,Sekta ya Fedha nchini imeendelea kuimarika na kufanya vema zaidi.
Ameyasema hayo Januari 19,2025 jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi Desemba,2024.
Ni mbele ya wajumbe ya wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM ambao umeongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Waziri Mkuu amesema,akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani bilioni 5.05, zikitosheleza uagizaji wa bidhaa kwa miezi 4.1.
Pia,mauzo ya bidhaa nje ya nchi yaliongezeka kutoka dola bilioni 8.81 mwaka 2020 hadi dola bilioni 14.66 mwaka 2024;
"Wastani wa mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania yameongezeka kutoka shilingi trilioni 1.47 Novemba, 2020 hadi shilingi trilioni 2.37 Novemba, 2024."
Amesema,madeni yaliyohakikiwa ya shilingi trilioni 3.47 yamelipwa kwa wakandarasi, watumishi, watoa huduma, wazabuni na madeni mengineyo ya kimkataba.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa, mikopo ya shilingi bilioni 693.9 ilitolewa na Serikali kwa wanufaika zaidi ya milioni 1.7 katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
"Na mtaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) umekua kutoka shilingi bilioni 60 mwaka 2020 hadi shilingi bilioni 438 mwaka 2024."
Katika hatua nyingine akizungumzia ushiriki wa Sekta Binafsi katika Uwekezaji amesema,
sheria 62 zimefanyiwa marekebisho, huku ada na tozo 374 zisizo na tija zikifutwa.
Amesema, Serikali imewezesha hayo ili kuhakikisha sekta hiyo inashiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo na uwekezaji.
Pia, amesema Mfumo wa Dirisha Moja umeunganishwa kwa kujumuisha taasisi saba za Serikali ili kurahisisha uwekezaji ambapo kwa sasa vibali vya uwekezaji vinapatikana ndani ya siku tatu;
"Miradi 1,282 yenye thamani ya dola bilioni 15.1 imesajiliwa na inatarajiwa kuzalisha ajira 248,309 na umeanzishwa mfumo maalum wa kuwezesha mifumo ya Serikali kuwasiliana na kubadilishana taarifa (Government Enterprise Service Bus - GovESB)."
Waziri Mkuu amesema, tayari jumla ya mifumo 80 kati ya mifumo 130 ya taasisi za umma imewezeshwa kuwasiliana na kubadilishana taarifa kidigitali.