NA GODFREY NNKO
SERIKALI imeendelea kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa sera, mikakati na programu ya maendeleo katika sekta ya maji.
Vilevile kuendeleza tafiti kuhusu teknolojia bora zinazotumika katika kutoa huduma ya maji na kusimamia matumizi endelevu ya rasilimali za maji.
Ameyasema hayo Januari 19,2025 jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi Desemba,2024.
Ni mbele ya wajumbe ya wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM ambao umeongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Waziri Mkuu amesema,kutokana na juhudi hizo, mafanikio mengi yamepatikana katika kipindi cha Novemba, 2020 hadi Novemba, 2024.Amesema,miradi 1,633 ya maji imetekelezwa, ikiwemo 1,335 ya vijijini na 298 ya mijini. Hii imeongeza upatikanaji wa maji vijijini kutoka asilimia 70.1 hadi asilimia 79.6 na mijini kutoka asilimia 84 hadi asilimia 90.
"Mradi mkubwa wa maji Arusha umeongeza uzalishaji kutoka lita milioni 40 hadi lita milioni 200 kwa siku na muda wa huduma umeongezeka kutoka saa 12 hadi 24."
Pia, amesema ujenzi wa miradi ya maji katika miji 28 inayogharimu shilingi trilioni 1.58 na kukamilika kwa miradi 218 kupitia fedha za Mpango wa UVIKO-19 umesaidia watu milioni 2.09. Chini ya mpango huo, miradi 44 imetekelezwa mijini na 174 vijijini.
Aidha, amesema Serikali imenunua na kuanza kutumika kwa seti 25 za mitambo ya kuchimba visima, seti tano za mitambo ya ujenzi wa mabwawa na seti nne za vifaa vya utafiti wa maji chini ya ardhi.
Mbali na hayo, Waziri Mkuu amesema, ujenzi wa Bwawa la Kidunda linalogharimu shilingi bilioni 329.46 umeanza ili kuhakikisha maji yanapatikana katika kipindi chote cha mwaka katika Mto Ruvu ambao ni chanzo kikuu cha maji kwa Jiji la Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Pwani.
Amesema,awamu ya kwanza ya Mradi wa Same Mwanga Korogwe umekamilika ambao umeanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi wapatao 450,000.
Mafanikio mengine amesema, ni kuwafikia wananchi milioni 4.07 walio vijijini kupitia programu ya PforR na kuongeza mikoa inayonufaika kutoka 17 hadi 25 na halmashauri kutoka 86 hadi 137.
Sambamba na kukamilika kwa uchimbaji wa visima 1,092 kwa ajili ya kutoa huduma ya maji katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na kuimarika kwa matumizi ya mifumo ya TEHAMA ili kuboresha huduma hizo nchini.