ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, miaka 61 ya Mapinduzi ni kumbukumbu ya wananchi wa Zanzibar kujikomboa kiuchumi, kisiasa na kijamiì yaliyotokana na madhila ya kutawaliwa.
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Januari 12,2025 alipowahutubia wananchi katika Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar katika Uwanja wa Gombani,Pemba.
Ameeleza kuwa, mafanikio makubwa yamepatikana katika kufikia malengo ya Mapinduzi ya Usawa, wananchi kuwa wanufaika wa rasilimali na fursa sawa bila upendeleo.
Rais Dkt.Mwinyi amebainisha kuwa, Serikali imeitafsiri dhana ya Mapinduzi kwa kuleta mageuzi ya kiuchumi,kisiasa na kijamii.
Aidha, ameeleza kuwa nchi imepata mafanikio makubwa katika kukuza uchumi, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kudhibiti matumizi yote.
Eneo jingine ambalo Dkt.Mwinyi amelielezea kuwa la mafanikio ni kuwawezesha wananchi kiuchumi, kuimarisha miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege,bandari, nyumba za makazi,miundombinu ya michezo, huduma za afya,umeme,elimu na kuimarisha demokrasia na utawala nora.
Halikadhalika amewasisitiza Wanasiasa, Viongozi wa Dini na Wananchi kuwa mstari wa mbele katika kudumisha amani na utulivu wa nchi ili maendeleo makubwa zaidi yapatikane.
Akizungumzia suala la uchaguzi, Dkt.Mwinyi amesema, ni wajibu wa kila mwananchi kuiombea nchi amani,utulivu na mshikamano ili hatimaye nchi ifanye Uchaguzi wa Kidemokrasia,Uwazi na Misingi ya Kisheria.
Aidha,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshiriki maadhimisho hayo, pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali kitaifa kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Vilevile,mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini, vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa dini na vyama vya siasa na wananchi kutoka mikoa ya Unguja na Pemba.