ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameeleza kuwa, Serikali inajipanga kwa ujenzi wa maghala ya kuhifadhia chakula ili kuwa na uhakika wa chakula hivyo kujitokeza kwa sekta binafsi kuanza kujenga ghala ni jambo linalopaswa kuungwa mkono.
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo alipofungua ghala la kuhifadhia chakula Gando, Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba linalomilikiwa na Kampuni ya Yasser Provision.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amesema, Serikali inalenga kuwapunguzia mzigo wa gharama wafanyabiashara wanaoleta chakula nchini ili kuwepo kwa unafuu wa bei kwa wananchi.
Rais Dkt.Mwinyi ameielezea njia nyingine ni kuwa na ushuru maalum kwa bidhaa zinazopelekwa Pemba.
Halikadhalika, Rais Dkt.Mwinyi amebainisha kuwa mpango wa kuifungua Pemba kiuchumi una dhamira thabiti ya kuhakikisha bei za bidhaa muhimu zinashuka na kutoa unafuu wa maisha kwa wananchi.
Amefahamisha kuwa, ujenzi wa bandari za Mkoani,Shumba Mjini na Wete ambao utaanza karibuni ni miongoni mwa hatua muhimu ya kuwawezesha wafanyabishara kuleta mizigo yao moja kwa moja Pemba kutoka nchi wanazoagiza ili kupunguza gharama za mzunguko wa usafirishaji.