ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema,Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wakubwa katika Sekta ya Uchumi wa Buluu ili nao wawasaidie wafugaji wadogo wadogo kuimarisha ufugaji wa Matango Bahari. .
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo alipozindua Mradi wa Visiwani Sea Cucumber Farm Zanzibar uliopo Ukunjwi Jimbo la Gando Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amesema Serikali imeweka mkazo katika sekta tatu katika Uchumi wa Buluu nazo ni Uvuvi, Ukulima wa Mwani na eneo la tatu ni Ufugaji wa Mazao ya Baharini ikiwemo Ufugaji wa Samaki ,Kaa Kamba na Matango Bahari.
Halikadhalika Rais Dk.Mwinyi amefahamisha kuwa lengo ni kuhakikisha Wawaekezaji Wakubwa wanawasaidia wafugaji wadogo kupata zana za kufanyia kazi hiyo pamoja na kuwapa Vifaranga na hatimae kununua Mazao ya Baharini kupitia Wafugaji hao Wadogo.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa,wawekezaji wakubwa katika Sekta Binafsi iwapo wataendelea na hatua waliofikia katika ufugaji wa Matango Bahari Zanzibar itakuwa Kinara wa Uzalishaji wa Matango Bahari.
Rais Dkt.Mwinyi amesisitiza kuwa, lengo la kuanzisha Wizara ya Uchumi wa Buluu ni kuhakikisha rasilimali za bahari zinatumika vyema na Kutoa ajira pamoja na nchi kunufaika jiuchumi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Mradi wa Visiwani Sea Cucumber Farm Zanzibar, Toufiq Salim TUrky amesema, taasisi hiyo inakusudia kujenga Kiwanda cha Kusarifu Matango Bahari Pemba pamoja na kuwa na lengo kuu la kuwawezesha wananchi wengine kufuga Matango Bahari ili kufikia lengo la kuzalisha tani 100 za Matango Bahari hapa nchini.