MARA-Serikali mkoani Mara ameishukuru Kampuni ya Umma ya HAIPPA PLC iliyoanzishwa Mkoani humo zaidi ya miaka miwili iliyopita kwa kuendelea kuwa chachu ya kuchangia ukuaji wa maendeleo hasa ushiriki wake kuwekeza, kufanya Uhamasishaji na Uelimishaji kwa Wananchi kujikita kufanya shughuli za Uwekezaji ili kuinua uchumi.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa huo Kanali Evans Mtambi Januari 30, 2025, kupitia hotuba yake iliyotolewa na Gambales Timotheo ambaye ni Mkuu wa Sehemu ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakati akifungua mkutano Mkuu maalumu wa utambulisho wa Huduma za HAIPPA PLC ndani ya Mkoa huo iliyofanyika katika ukumbi wa MCC uliopo Mjini Musoma.
Kupitia hotuba hiyo Kanali Mtambi amesema, anafarijika kuona Kampuni ya Umma ya HAIPPA PLC ikitembea katika agenda ya maendeleo hasa Uwekezaji ambao unafaida kubwa kwa maendeleo ya Wananchi na Mkoa na hivyo kuwataka wananchi na Wafanyabiashara kutumia Soko la Hisa la HAIPPA PLC kujiinua kiuchumi.
Amesema hatua hiyo ni ya kuungwa mkono na wadau wengine huku pia akiihimiza izidi kutoa elimu kwa Wananchi na wadau mbalimbali kujitokeza kuwekeza mkoani humo kwa kutumia vyema Ziwa Victoria na ardhi nzuri kufanya shughuli za kilimo Biashara na ufugaji wa kisasa.
Aidha amesema, Serikali itaendelea kushirikiana na Kampuni hiyo kuweza kuwafikia Wananchi wengi zaidi, huku akisisitiza kwamba wadau wote waendelee kuwa Mabalozi wa kutangaza huduma zinazotolewa kwani zina faida moja kwa moja kwa Wananchi kuwasaidia kupata maendeleo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Umma ya HAIPPA PLC Boniphace Ndengo amesema kuwa, Kampuni hiyo ilianzishwa Octoba 27, 2022 ikiwa na Wanahisa Waanzilishi nane ambapo walianza na Mtaji wa Mil. 3.
Huku njozi ya kuanzishwa kwake ni kuwa akademi bora ya Uwekezaji Tanzania na Afrika. Na dhamira ikiwa ni kubuni, kujenga,kuwekeza na kuwezesha miradi mikubwa ya Afrika.
Amesema Kampuni hiyo ilisajiliwa kutengeneza mtaji wa Bil. 500, ambapo hadi Sasa mtaji wa Mil. 290, umelipwa na baada ya miaka 10 Kampuni hiyo inatarajia kufikia kiwango hicho na kwa sasa imesajili Wanahisa 456, na inatoa gawio la asilimia 35 kwa mwaka. Huku Kampuni hiyo imefanikiwa kuanzisha Kampuni tanzu tatu na kujenga Soko la Kampuni hiyo kidigitali ili kuwafikia watu wengi zaidi.
"Kampuni ya HAIPPA PLC inatoa huduma za ujenzi wa makampuni ya umma na makampuni ya Uwekezaji, urasimishaji,Uanzishaji na uendelezaji wa Biashara, ujenzi wa mitaji, huduma za masoko, ujenzi wa Miundombinu ya mifumo ya Biashara, kuelimisha na kuwezesha umma kushiriki kwenye miradi mikubwa ya Uwekezaji kupitia Kampuni za Umma na Ubia Kati ya Serikali na Sekta binafsi."amesema Ndengo.
Amesema Malengo ya HAIPPA PLC kwa mwaka 2025-2029 ni kutumia Teknolojia ya Mawasiliano ya Ushirikiano na Wadau mbalimbali kuwafikia wa-Tanzania Mil. 20,ili kuwapa elimu ya Uwekezaji hususan Uwekezaji kupitia Kampuni za Umma. Na kuwezesha Uanzishaji wa Kampuni za Umma angalau 50.
Pia, kuwezesha angalau Watanzania Mil. 6, kushiriki Uwekezaji mkubwa kupitia Kampuni za Umma na Miradi ya PPP. Na pia kukuza kipato cha Mtanzania (GDP per Capital) aliyemwekezaji wa HAIPPA kutoka Wastani wa Shilingi Mil. 3, kwa mwaka hadi Shilingi Mil. 30 ifikapo 2028.
Aidha, amesema HAIPPA PLC kwa sasa imejipanga vyema kushirikiana na Viongozi wa serikali za mitaa Mkoani Mara kuangalia fursa gani wanaweza kubuni katika maeneo yao na kuzianzisha kusudi zisaidie kuchangia uchumi wa Wananchi katika maeneo yao kwa kuwekeza kikamilifu.
Katika mkutano huo, Wanahisa wamepitisha mapendekezo ya bodi kuuza hisa Mpya kwa Wanahisa wapya kwenye Umma na kutoa hisa satahiki kwa Wanahisa Waanzilishi.