NA GODFREY NNKO
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imerekodi mafanikio makubwa katika sekta ya michezo nchini.
Ameyasema hayo Januari 19,2025 jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi Desemba,2024.
Ni mbele ya wajumbe ya wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM ambao umeongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
"Michezo ni muhimu katika kujenga utambulisho wa kitaifa na mshikamano wa kijamii. Mafanikio yaliyopatikana kwenye sekta ya michezo ni mengi, lakini kwa uchache ni haya yafuatayo:
"Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikisisitiza wananchi wajali afya zao kwa kufanya mazoezi mara kwa mara angalau kila Jumamosi."
Waziri Mkuu amesema,kutokana na jitihada hizo, vilabu 692 vya michezo vimeanzishwa, huku vilabu 115 vya mbio za polepole (jogging) vikisajiliwa katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Pia, amesema mchezo wa mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu Tanzania umepanda viwango katika historia ya michezo hapa nchini kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita.
"Timu ya mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu ya Tembo Warriors, kwa mara ya kwanza ilishiriki na kufanikiwa kufika hatua ya robo fainali za Kombe la Dunia nchini Uturuki mnamo Septemba, 2022 na kuiweka nchi yetu katika nafasi ya saba kati ya timu 10 bora za dunia.
"Timu ya Soka ya Wanawake (Twiga Stars) imefuzu kwa mara ya kwanza kushiriki mashindano ya fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa Wanawake (WAFCON).
"Timu za Tanzania za vijana chini ya miaka 20 zimetwaa ubingwa wa CECAFA na chini ya miaka 15 ubingwa wa michuano ya timu za Taifa za Africa (African Schools Footbal Championship)."
Amesema,Tanzania kupata fursa ya kuwa mwenyeji wa AFCON 2027, hiyo ni mara ya kwanza tangu nchi ipate uhuru.
Vilevile, amesema ujenzi na ukarabati mkubwa wa miundombinu ya michezo ikiwemo kuanza ujenzi wa uwanja mpya wa Arusha ambao umefikia karibu asilimia 20 ya utekelezaji.
"Ninakupongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM kwa kutoa motisha kwa vilabu vya ndani vinavyoshiriki mashindano ya kimataifa kupitia Goli la Mama na Knock Out ya Mama kwenye masumbwi.
"Kwa mara ya kwanza Tanzania Bara imeweza kuingiza timu nne mfululizo kwenye mashindano ya ngazi ya vilabu barani Afrika hadi mwaka 2024/2025.
"Timu ya Wananchi -Yanga imefanikiwa kufika ngazi ya Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika.
"Kuingiza timu mbili za Simba na Yanga kwa pamoja kwa mara ya kwanza mwaka 2023/2024 kuweza kucheza ngazi ya robo fainali ya mashindano ya Klabu Bingwa barani Afrika."