Serikali yapiga hatua udhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele huku ikihitaji mshikamano zaidi

DAR-Serikali imesema kuwa, imepiga hatua kubwa katika juhudi za kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele nchini huku ikiendelea kuwahimiza wanajamii kuendelea kuzingatia kanuni na taratibu za afya.
Magonjwa hayo yanajumuisha ugonjwa wa matende na mabusha, trakoma, usubi,minyoo ya tumbo na kichocho.

Kaimu Meneja wa Mpango wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDCP) kutoka Wizara ya Afya, Dkt.Faraja Lyamuya ameyasema hayo leo Januari 21,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari.
Mafunzo hayo kwa waandishi wa habari ni mahususi kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele Duniani ambayo kilele ni Januari 30,2025 huku kauli mbiu ikiwa ni "Tuungane,Tuchuke hatua, Tutokomeze Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele."

Dkt.Lyamuya amesema,halmashauri 114 nchini zimeacha kugawa kinga tiba za ugonjwa wa matende na mabusha kutokana na mafanikio ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Vilevile amewataka wanajamii kuepukana na imani potofu kuhusu magonjwa hayo hususani wale ambao wanaamini kuwa yanatokana na kulogwa au kurithi.

"Sio kweli kwamba ugonjwa wa matende na mabusha au ngiri maji huambukizwa kwa kunywa maji ya madafu, wala si ugonjwa wa kulogwa.
"Sio kweli kwamba ni ugonjwa unaothiri ukanda wa Pwani pekee bali maeneo yote yenye mbu wenye vimelea watu wanaweza kupatwa na huu ugonjwa,"amesema Dkt.Lyamuya.

Katika hatua nyingine, halmashauri ambazo zinaendelea na ugawaji wa kinga tiba ni tano ikiwemo Manispaa ya Kinondoni iliyopo mkoani Dar es Salaam, Lindi na Mtama za mkoani Lindi, Pangani mkoani Tanga na Mikindani.

Afisa Mpango, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDCP), Dkt. Lilian Ryatura amesema, halmashauri zilizokuwa na maambukizi ya juu ya zaidi ya asilimia tano ya ugonjwa wa Trachoma zilikuwa ni 69.

Dkt.Ryatura amesema, baada ya kutoa kingatiba aina ya Zithromax zimepungua hadi kufikia halmashauri tisa pekee.

Halmashauri hizo kuwa ni Longido, Ngorongoro, Monduli, Kiteto, Simanjiro, Kalambo, Mpwapwa, Kongwa na Chamwino huku akisisitiza kuwa ugonjwa huo hutibika kwa mtu kufanyiwa upasuaji mdogo wa kusawazisha kope.

"Ugonjwa huu usipotibiwa mapema unaweza kusababisha uoni hafifu,na hatimaye ulemavu wa kutokuona au upofu usiotibika."
Mbali na hayo,Afisa Mpango, Dkt.Mohamed Nyati ameishauri jamii kumeza kingatiba ya Kichocho kila zinazotolewa kwenye jamii na shuleni kama njia kujikinga na ugonjwa huo.

Dkt.Nyati ameizitaja njia nyingine za kujikinga na ugonjwa huo kuwa ni pamoja na kutumia choo kw haja kubwa na ndogo, kuepuka kufua, kuogelea, au kuosha vyombo ndani ya maji yaliyotuama kama mabwawa, madimbwi na ziwani.
Naye Ruth Mchomvu ambaye ni Afisa Mpango, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDCP) amesema, watu zaidi ya milioni 7.2 wanaoishi katika mikoa ya Morogoro, Ruvuma, Mbeya, Songwe, Tanga, Iringa, Njombe, Iringa na Dodoma wako hatarini kupata ugonjwa wa Usubi, ugonjwa ambao unaweza kutibika na kuzuilika.

Mchomvu amesema, ni muhimu kwa wananchi kumeza kingatiba za ugonjwa huo kila zinapotolewa kwenye jamii kwa kuwa dalili za ugonjwa huo huwa hazijtokezi mapema.
Naye Afisa Mpango Catherine Mahimbo amesema,ugonjwa huo unaathiri watu wa rika zote wakiwemo watu wazima katika jamii na usipotibika mapema husababisha madhara mengi ikiwemo kupungua kwa damu, utapiamlo, kupungua uzito,udumavu wa akili na mwili kwa watoto.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news