Serikali yawataka watoa huduma za fedha kufuata sheria na taratibu za BoT

NA ASIA SINGANO
WF

WATOA huduma za fedha nchini wametakiwa kufuata Sheria na taratibu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ikiwemo kujisajili, kutoza viwango sahihi vya riba na kuwapa nakala za mikataba wakopaji baada ya wao kuelewa mkataba wa makubaliano ya kukopa na kusaini ili kuepuka adhabu mbalimbali zitakazotolewa kwa wanaokiuka Sheria za huduma za fedha.
Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Bw. Selemani Msumi, Ofisini kwake wakati Timu ya Walaam wa kutoa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha na taasisi zake walioambatana na Maafisa wengine (hawapo pichani) walipomtembelea ofisini kwake kabla ya kuelekea Kata za Ilikiding’a na Kata ya Kiranyi kutoa elimu ya fedha kwa wajasiliamali na wananchi wa kata hizo pamoja na maeneo jirani.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Bw. Selemani Msumi, ofisini kwake alipokutana na kufanya mazungumzo na Timu ya Wataalamu wa kutoa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha na taasisi zake pamoja na wadau mbalimbali.
Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Bw. Selemani Msumi, Nyenzo ya kufundishia elimu ya fedha wakati Timu ya Walaam wa kutoa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha na taasisi zake walioambatana na Maafisa wengine wa Serikali (hawapo pichani) walipomtembelea ofisini kwake kabla ya kuelekea Kata za Ilikiding’a na Kiranyi kutoa elimu ya fedha kwa wajasiliamali na wananchi wa kata hizo pamoja na maeneo jirani.

Alisema kuwa Serikali inaendelea kufanya uchunguzi kuwabaini wanaofanya biashara ya kutoa huduma za fedha bila leseni, huku akisisitiza kuwa watakaobainika kukiuka Sheria na taratibu za huduma ndogo za fedha hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Bw. Selemani Msumi (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Wataalam wa kutoa Elimu ya Fedha, Kutoka Wizara ya Fedha na taasisi zake, kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha, Afisa Usimamizi wa Fedha Mwandamizi, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro (wapili kulia), Mchumi, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Godfrey Mwatwinza (wakwanza kushoto) pamoja na Afisa Mwandamizi, Uchambuzi Fedha, Idara ya Sera, Utafiti na Mipango, kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA. Gladness Mollel (wapili kushoto).

‘’Mtu yeyote anayeendesha biashara ya kukopesha pasipo kufuata taratibu, pasipokuwa na leseni hilo ni kosa na ni wizi kama wizi mwingine, tumeshaanza oparesheni ya kuhakikisha wanaokopesha bila kuwa na leseni na ambao hawafuati Sheria na taratibu tunawakamata’’ alisema Bw. Msumi.
Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, akitoa ufafanuzi kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wa Kata ya Ilikiding’a katika Shule ya Sekondari Ilikiding’a, Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, kuhusu filamu ya elimu ya fedha yenye ujumbe kuhusu masuala ya uwekezaji, utunzaji wa fedha binafsi, kuweka akiba, kusajili vikundi vidogo vya fedha pamoja na masuala ya mikopo ambapo Timu ya Wataalam wa elimu wa fedha wanaendelea kutoa elimu ya fedha katika mkoa huo.

Akitoa elimu ya fedha kwa wajasiliamali na wananchi wa Kata ya Ilikiding’a katika Shule ya Sekondari Ilikiding’a, Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw Salim Kimaro amewataka wajasiliamali hao kusajili vikundi vyao vya huduma ndogo za fedha ili kulinda fedha zao dhidi ya wanakikundi wasiyo waaminifu.
Baadhi ya wajasiriamali na wananchi wa Kata ya Ilikiding’a katika Shule ya Sekondari Ilikiding’a, Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, wakipata elimu ya fedha kwa njia ya filamu yenye maudhui kuhusu matumizi sahihi ya fedha, umuhimu wa kupanga bajeti na kuitekeleza, umuhimu wa kusajili vikundi vya huduma ndogo za fedha , utunzaji wa fedha binafsi, umuhimu wa kushirikisha familia na watu wa karibu kwenye masuala ya fedha na uwekezaji, umuhimu wa kukata bima ya biashara na mali nyingine, filamu hiyo imeandaliwa na Wizara ya Fedha lengo likiwa ni kusambaza elimu ya fedha kwa njia rahisi ya burudani ili kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa masuala ya huduma za fedha.

‘’Hatusemi vile vikundi vyenu ambavyo havijasajiliwa mvivunje hapana, ni vizuri ila nendeni mkavisajili, kama wale mliowaona kwenye filamu wangesajili kikundi chao na kuweka hela benki fedha zao zisingepotea,’’ alisema Bw. Kimaro.

Kwa upande wake Bw. Lulu Mesikana, ambaye ni mmoja wa wajasiliamali waliohudhuria mafunzo hayo ya elimu ya fedha, aliipongeza Wizara ya Fedha kwa kuona umuhimu wa kutoa elimu hiyo kwa wananchi huku akiomba programu hiyo ya elimu ya fedha iwe endelevu.
Mchumi, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Godfrey Mwatwinza, akigawa vipeperushi vyenye ujumbe kuhusu masuala ya fedha na uwekezaji kwa wajasiliamali na wananchi wa Kata ya ya Kiranyi wilayani Arusha mkoani Arusha, ili waendelee kujikumbusha kuhusu mafunzo ya elimu ya fedha waliyopewa na wataalam hao na kuendelea kueneza elimu hiyo kwa familia zao na wananchi wengine waliyoshindwa kufika kutokana na sababu mbalimbali.

‘’Tunashukuru sana kwa semina hii na tukitoka hapa sasa tutakuwa makini na tutalinda fedha zetu ili tusipate hasara kama walivyoibiwa fedha wale tuliowaona kwenye filamu ya elimu ya fedha,"alisema Bw. Mesikana.

Naye Afisa Mwandamizi, Uchambuzi Fedha, Idara ya Sera, Utafiti na Mipango, kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA. Gladness Mollel, amewashauri wajasiliamali hao kuwekeza katika njia mbalimbali ikiwemo zile walizofundihswa na watalam wa elimu ya fedha kwa ajili ya kujikimu katika kila hali ya maisha.
Afisa Mwandamizi, Uchambuzi Fedha, Idara ya Sera, Utafiti na Mipango, kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA. Gladness Mollel, akitoa elimu kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wa kata ya Kiranyi Halmashauri ya Wilaya ya Arusha mkoani Arusha, kuhusu masuala ya uwekezaji alipoambatana na Maafisa kutoka Wizara ya Fedha, kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha, programu ambayo imeandaliwa na Wizara ya Fedha ikiwa ni awamu ya tatu ya program hiyo yenye lengo la kuwaelimisha wananchi wote juu ya masuala ya fedha.(Picha na Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini, WF - Arusha).

‘’Kuna njia nyingi za uwekezaji ikiwemo hatifungani kuna aina mbalimbali za hatifungani, kwanza zipo hatifungani za Serikali na pia zipo hatifungani za kampuni na taasisi nyingine,’’ alisema Bi. Gladness.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news