NA GODFREY NNKO
WIZARA ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Tume ya TEHAMA nchini kwa kushirikiana na SoftVentures,Chama cha Watoa Huduma za Mtandao Tanzania (TISPA) imetambulisha rasmi Mashindano ya Tuzo za TEHAMA 2025.
Wabunifu katika TEHAMA na wadau wengine nchini wanapata fursa ya kuwasilisha bunifu na kazi zao kuanzia sasa hadi Februari 10,2025 na zitafanyika Februari 21, 2025 katika Jengo la PAPU jijini Arusha.
Hayo yamesemwa leo Januari 24,2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga wakati akizungumza na wanahabari makao makuu ya tume jijini Dar es Salaam.
Amesema,Tuzo za TEHAMA 2025 zinalenga kutambua mchango mkubwa katika sekta ya TEHAMA ya Tanzania kwa kuwatambua watu binafsi,mashirika na miradi inayochochea mabadiliko ya kidigitali,kuimarisha ubunifu na kukuza ushirikishwaji.
"Hafla hii itakuwa jukwaa muhimu kwa viongozi wa sekta, watunga sera,na wabunifu kushirikiana, kuungana, na kuharakisha ukuaji wa uchumi wa kidigitali nchini."
Pia, ametoa wito kwa wabunifu,wadau wa TEHAMA, startups, taasisi za sekta ya umma na binafsi na mashirika yote Tanzania kushiriki kwenye tuzo za mwaka huu kwa kuwasilisha uteuzi wao katika vipengele mbalimbali. Miongoni mwa vipengele hivyo, Dkt.Mwasaga amesema ni;
1.Ubunifu katika Bidhaa au Huduma za TEHAMA
2.Matumizi Bora ya TEHAMA
3. TEHAMA kwa Maendeleo ya Jamii4.Kijana Aliyefanikiwa Katika TEHAMA
5.Wanawake Katika TEHAMA
6.Usalama wa TEHAMA
7. Mradi wa TEHAMA wa Sekta ya Umma
8.TEHAMA Endelevu
9.Tuzo za TISPA kwa Mtoa Huduma Bora ya Uunganishaji wa Mtandao
10.Tuzo Maalum ya Maisha kwa Mchango wa TEHAMA kutoka Wizara ya Mawasiliano,na Teknolojia ya Habari
Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, jumla ya tuzo 22 zinazotolewa, kila moja ya kipengele kilichoorodheshwa hapo juu kinabeba idadi ya vipengele vidogo vinavyowakilisha sekta na tasnia mbalimbali.
"Uteuzi uko wazi hadi tarehe 10 Februari 2025, na unaweza kuwasilishwa kupitia www.tehamaawards.tz."
Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Mifumo na Huduma za TEHAMA kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohamed Mashaka amesema,Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ilianzishwa Desemba, 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema,lengo kuu la wizara hiyo ni kutunga na kusimamia utekelezaji wa sera zinazohusu mawasiliano, teknolojia ya habari na huduma za posta, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuendeleza mabadilikoya kidijitali.
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inasimamia utekelezaji wa mkakati wa uchumi wa kidijitali kwa kushirikisha sekta za umma na binafsi.
"Mkakati huu unahamasisha uwepo wa program mbalimbali zinazokuza ubunifu, uundaji wa majukwaa na mifumo inayoboresha utoaji huduma katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii."
Mbali na hayo, Dkt.Mwasaga amesema,Tume ya TEHAMA ni taasisi ya umma inayohusika na utekelezaji wa sera na mikakati ya TEHAMA nchini Tanzania.
"Kwa kukuza uvumbuzi, utafiti, na ujenzi wa uwezo, Tume inachukua jukumu muhimu katika kuharakisha uchumi wa kidigitali na maendeleo ya kiteknolojia ya nchi."
Afisa Miundombinu TISPA, Joseph Rwegoshora amesema, Chama cha Watoa Huduma za Mtandao Tanzania (TISPA) ni chombo cha sekta kinacho wakilisha watoa huduma za mtandao na wadau wa TEHAMA.
Vilevile, TISPA inatetea ushirikishwaji wa kidigitali, maendeleoya sera, na upanuzi wa miundombinu ya TEHAMA ili kusaidia ukuaji wa uchumi wa kidigitali nchini Tanzania.
Mwanzilishi wa Kampuni ya SoftVentures ambao walileta wazo la tuzo hizo, Daniel Mhina amesema wanafurahi kuaminiwa na Wizara kupitia Tume ya TEHAMA katika ushirikiano huo wa kuandaa Tuzo za TEHAMA 2025.
Amesema, SoftVentures ni kampuni inayotegemea ubunifu, ikilenga kutumia teknolojia kama nyenzo ya kufanikisha maendeleo endelevu.
Pia, amesema kwa azma ya kuunda suluhisho zenye athari chanya, SoftVentures inawezesha jamii na kuimarisha ushirikiano kupitia TEHAMA.
"Kampuni hii inaweka mkazo katika kubuni suluhisho bunifu zinazotokana na mahitaji ya jamii, kukuza uchumi wa mzunguko katika sekta ya TEHAMA na kuhamasisha maendeleo endelevu."
Mhina amesema,kupitia ushirikiano na wadau muhimu,SoftVen-tures inajenga daraja kati ya teknolojia na maendeleo endelevu, ikihakikisha matokeo yanayooneka-na ndani ya Tanzania na nje ya mipaka yake.