PWANI-Serikali ya Mkoa wa Pwani imekamata shehena ya miundombinu ya Serikali iliyokuwa imeibiwa na kuhifadhiwa katika kiwanda cha kutengeneza vifaa vya ujenzi kilichopo Mkuranga.
Miundombinu hiyo, inayohusisha mali za Tanesco, Dawasa, na Shirika la Reli Tanzania (TRC), ilipatikana baada ya kikosi kazi maalum kuundwa kufuatilia uharibifu katika taasisi hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, akiwa na viongozi wengine wa mko na wilaya Januari 2, 2025, alikagua miundombinu hiyo katika kiwanda cha LN Feature Building Material.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kunenge alieleza kusikitishwa na baadhi ya wananchi wanaohujumu juhudi za serikali katika kuboresha miundombinu kwa kuiba na kuhifadhi vifaa hivyo.
Pia alisisitiza kuwa serikali haitavumilia vitendo vya aina hiyo na itaendelea kufuatilia na kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika.