ZANZIBAR-Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Riziki Pembe Juma amewataka waratibu wa wanawake na watoto na Masheha kuhakikisha wanasimamia ipasavyo suala zima la uanzishwaji wa majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi katika shehia zao, ili waweze kunufaika na Mradi wa Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi unaotarajiwa kuanza hivi karibuni kupitia Wizara hiyo.
Mhe. Riziki ameyasema hayo wakati alipofungua Mafunzo ya uanzishwaji wa Majukwaa ya uwezeshaji wa Wanawake kiuchumi kwa Masheha na waratibu wa wanawake na watoto wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema, lengo la kuanzishwa majukwaa hayo ni kuwaweka pamoja wanawake kishehia na kuanzisha vikundi vya ushirika, kuvisajili pamoja na kuzungumzia fursa mbalimbali za kuwawezesha wanawake kiuchumi ili waondokane na utegemezi.
Amesema, hatua hiyo ni miongoni mwa juhudi za Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzanzia, Dkt.Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika kuona wanamke wanainuka kiuchumi.
Amesema, viongozi hao wamekuwa wakitoa fursa nyingi katika kuwasaidia wanawake kuondokana na utegemezi, lakini haziwafikii ipasavyo, hivyo amesema imani yake ni kuwa kuanzishwa kwa majukwaa hayo yatasaidia kuwafikia fursa hizo kama zilivyokusudiwa.
"Katika shehia zenu mnajuana, hivyo ni vyema kuhakikisha mnashirikiana na mnaweka mikakati imara katika kuwasimamisha wanawake waliopo ndani ya shehia zenu ili muweze kufaidika na fursa zitakazotolewa na sio kuwaingiza wasiohusika na shehia," amesisitiza Mhe.Riziki.
Aidha,Mheshimiwa Riziki amewashukuru kwa uwepo wao na kuwataka kuendelea kupambana na masuala yote ya kijamii ili kuhakikisha wanatimiza malengo yao.
Amesema, furaha ya Serikali ni kuona kila kilichopangwa kiwafikie wananchi kinawafikia na kuwanufaisha.
Akiwasilisha muongozo wa majukwaa ya uwezeshaji wa wanawake kiuchumi katika ngazi ya Shehia, Afisa Jinsia kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto,Bw.Mohammed Jabir amesema imeonekana kuna baadhi ya vikundi kuwepo kwa tatizo la kupigwa danadana juu ya kupata usajili wa vikundi vyao, hali ambayo inarudisha nyuma juhudi za ukuaji wa uchumi.
Wakitoa michango yao, baadhi ya waratibu na masheha wamesema, kuna changamoto kubwa kwa baadhi ya wana vikundi kutokuwa na elimu ya kujua kusoma wala kuandika, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu ya kutosha ili malengo ya kuanzishwa majukwaa hayo yaweze kufikiwa.