NA DIRAMAKINI
SIMBA Sports Club ya jijini Dar es Salaam imechukua alama tatu ugenini dhidi ya CS Sfaxien kukwea kileleni mwa msimamo wa Kundi A la Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAFCC).

Aidha,CS Sfaxien ambao mwishoni mwa mwaka jana waliwafanyia fujo Simba SC katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam wameondolewa rasmi kwenye kinyang'anyiro cha kwenda robo fainali.
Simba SC imepata ushindi huo katika mchezo wa Kombe la Shirikisho barani Afrika uliopigwa Uwanja wa Hammadi Agrebi nchini Tunisia.

Jean Charles Ahoua aliwapatia Simba SC bao hilo pekee dakika ya 34 kwa shuti kali akiwa ndani ya 18 baada ya kumalizia pasi ya Leonel Ateba kufuatia mpira mrefu uliopigwa na Che Fondoh Malone.

Ushindi wa leo umewafanya kufikisha alama tisa na kuwa vinara wa kundi baada ya kucheza mechi nne.

Kocha Fadlu amemuanzisha Leonel Ateba akichukua nafasi ya Steven Mukwala ambaye ameanzia benchi.

Wachezaji wa Akiba:
Ally Salim (1), Kelvin Kijili (33), Karaboue Chamou (2), Augustine Okejepha (25), Mzamiru Yassin (19), Ladaki Chasambi (36), Debora Fernandes (17), Steven Mukwala (11), Awesu Awesu (23).