ZANZIBAR-Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango,Dkt.Saada Mkuya Salum amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inahakikisha inaboresha miundombinu ya barabara kwa wananchi mjini na vijijini ili kurahisisha huduma za kijamii.
Ameyasema hayo Mpendae wakati akiweka Jiwe la Msingi katika Barabara ya Mpendae Planed Area Street Road yenye urefu wa kilomita 6.41 ikiwa ni shamrashamra za kutimiza miaka 61 ya Mapinduzi.
Aidha, amesema kuwa lengo la Serikali kuhakikisha barabara zote za Zanzibar zinajengwa kwa kiwango cha lami na kusema kuwa watahakikisha barabara zote zinakamilika kwa kiwango hicho ikiwemo na zile zinaendelea kujengwa ili kuleta maendeleo kwa wananchi.
Amesema, ni ujenzi wa barabara hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika kutekeleza ahadi zake alizozitoa kwa wananchi wake.
"Tunajua kwamba unatekelezea ilani ya chama na una wasimamimizi wako ambao wanasimamia ilani hiyo,"alisema Waziri.
Hata hivyo amewataka madereva na watumiaji wengine kuitumia barabara hiyo kwa usalama zaidi ili kupunguza ajali zinazoweza kuepukika.
Akitoa taarifa ya kitaalamu kuhusu barabara hiyo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Hawaa Ibrahim Mbaye amesema kuwa, eneo la Mpendae limebahatika mradi wa barabara za Mjini zenye urefu wa kilomita 157 ambazo zinajengwa na Mkandarasi kutoka China (CCECC).
Aidha amefahamisha kuwa ujenzi hiyo umezingatia madaraja, miundombinu ya kupitisha maji ya mvua, njia za watembeza kwa miguu, alama za usalama barabarani, taa, pamoja na kuzingatia mahitaji ya watu wenye mahitaji maalum.