Stephen Wasira ndiye Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara

DODOMA-Kada mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira amechaguliwa kwa kura za kishindo kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Taifa unaoendelea jijini Dodoma leo Januari 18, 2025.

Katika mkutano huo, kura 1921 zimepigwa, ambapo kura halali zilikuwa 1917. Kura za hapana zilikuwa saba, na kura za ndiyo zilikuwa 1910,sawa na asilimia 99.42 huku kura nne zikiharibika.
Awali,jina la Wasira limewasilishwa mbele ya Mkutano Mkuu na limepata baraka za Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho, kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Abdulrahman Kinana, ambaye alitangaza kupumzika miezi mitano iliyopita.

Stephen Wasira ni nani?

Stephen Wasira alizaliwa mwaka 1945 katika Wilaya ya Bunda, Mkoa wa Mara ana miaka 80. Alisoma katika shule tatu tofauti, ya kwanza ni Shule ya Msingi Bariri 1956-1959, ya pili ni Shule ya Msingi Nyambitilwa 1960–1961 na kisha akamalizia Shule ya Msingi Kisangwa mwaka 1962 - 1963.

Kati ya mwaka 1964–1967, Wasira alisoma elimu ya Sekondari katika Chuo cha Ukufunzi Uingereza (British Tutorial College) na kuhitimu kidato cha nne.

Wakati anasoma sekondari (1965–1967), pia alifanya kazi akiwa msaidizi wa masuala ya maendeleo ya jamii na alipohitimu kidato cha nne alianza kuitumikia Tanu akiwa katibu wa wilaya mwaka 1967-1973.

Mwaka 1975–1982 alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara na mwaka 1982 akateuliwa kuwa Ofisa Mwandamizi katika Ubalozi wa Tanzania Washington, D.C. Alipokuwa huko alisoma na kuhitimu Shahada ya Kwanza ya Uchumi na Uhusiano ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Amerika (American University) kilichopo Washington DC mwaka 1982–1985.

Wasira alisoma Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Umma kati ya mwaka 1985–1986 na aliporejea nchini kuendelea na utumishi wa uwakilishi wa wananchi, aliteuliwa na Rais Ali Hassan Mwinyi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani mwaka 1990-1991.

Kati ya mwaka 1993–1995 alisoma tena Shahada ya Uzamili ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Amerika.

Mwaka 1985 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Bunda, baada ya jimbo hilo kugawanywa na Mwibara, ambapo Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi alimteua kuwa Naibu wa Waziri wa Serikali za Mitaa na baadaye Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo.

Mwaka 1995 Wasira aliwania ubunge wa Bunda kupitia CCM, lakini alishindwa kwenye kura za maoni na Joseph Warioba, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu, hivyo Wassira akaondoka CCM na kuhamia Chama cha NCCR Mageuzi. Alipeperusha bendera ya chama hicha katika uchaguzi wa ubunge na kumuangusha Warioba.

Hata hivyo CCM kupitia mgombea wake, Jaji Warioba ilipinga matokeo hayo mahakamani ambako Mahakama Kuu Mwanza ilitengua ubunge wa Mzee Wasira. 

Uchaguzi wa marudio ulifanyika mwaka 1999 na baada ya uchaguzi huo Wasira alijiunga tena na CCM.

Uchaguzi wa mwaka 2005 alijitosa Jimbo la Bunda na alishinda kura za maoni ndani ya CCM na kuwa mgombea katika jimbo hilo ambako katika Uchaguzi Mkuu alipita bila kupingwa, akatangazwa kuwa mbunge.Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Maji Januari 2006- Oktoba 2006.

Kati ya Novemba 2006 hadi Novemba 2010 alikuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, lakini Februari–Mei 2008 aliwahi kutumikia kwa muda Ofisi ya Waziri Mkuu akiwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Uchaguzi wa mwaka 2010, Wasira aligombea tena ubunge wa Bunda na kushinda kwa asilimia 66.1 na Rais Kikwete akamteua kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Uhusiano na Uratibu kabla ya kurudishwa kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.

Pia amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama, ikiwemo Mjumbe wa Kamati Kuu na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC). Alikuwa miongoni mwa wana CCM waliochukua fomu kuomba kuteuliwa kuwania urais mwaka 2015, ambapo Dkt. John Magufuli aliteuliwa kupeperusha bendera ya CCM.

Dkt.Samia Suluhu Hassan 

Awali Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekemea baadhi ya wanachama wa CCM wenye tabia ya kuendeleza makundi katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu badala ya kuwaunga mkono wagombea waliopitishwa na chama.

Ametoa onyo hilo leo Januari 18,2025 wakati akizungumza na maelfu ya wajumbe, viongozi wakuu, wastaafu, mabalozi na wageni kutoka vyama rafiki wakati akifungua Mkutano Mkuu Maalum wa CCM uliofanyika jijini Dodoma.

Dkt.Samia amesema kuwa, wapo baadhi ya wanaCCM wamekuwa wakiendeleza makundi ya uchaguzi licha ya Chama kupitisha jina la mgombea.

“Teueni wagombea wanaokubalika na kutounda makundi, tunasema makundi ndani ya chama wakati wa kuomba ni kwa sababu ya demokrasia, kwani waombaji ni wengi hivyo tutapata makundi. Lakini tutakaposimamisha wagombea wa chama chetu tunaomba makundi yasiendelee."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news