DODOMA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema katika muongo mmoja uliopita, Tanzania imepiga hatua katika kuboresha huduma za afya kwa jamii katika sekta ya afya.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus wakizungumza na waandishi wa habari Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo Januari 20, 2025.
Rais Dkt.Samia ameyasema hayo leo wakati yeye na mgeni wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO),Dkt. Tedros Ghebreyesus wakizungumza na vyombo vya habari, Ikulu Chamwino jijini Dodoma.
Aidha, Rais Samia amesema juhudi za Serikali katika kupunguza vifo vya wajawazito zimesaidia kutoka vifo 556 hadi vifo 104 kwa kila vizazi hai 100,000.
Hali kadhalika, Rais Dkt. Samia amesema jitihada hizo zimechangiwa na Serikali kuwekeza katika miundombinu ya afya ambapo imewezesha asilimia sabini ya wananachi kuweza kupata huduma za afya ya msingi ndani ya umbali wa kilomita tano.
Rais Dkt. Samia pia amesema vifo vya Watoto chini ya umri wa miaka mitano vimepungua kutoka asilimia sitini na saba hadi asilimia arobaini na tatu kati ya vizazi hai 1,000.
Hata hivyo, vifo vya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati vimepungua kwa kasi ndogo.
Vile vile, Rais Dkt. Samia amasema,Tanzania inafungamana na mapendekezo ya WHO kuanzisha vitengo vya kuhudumia watoto wachanga hususan wanaozaliwa kabla ya muda hadi kufikia asilimia themanini ya vituo vinavyotoa huduma za afya.
Mwaka 2024 Tanzania ilipiga hatua muhimu katika kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa watu wote kwa kuzindua mpango jumuishi na shirikishi wa wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii utakaowafikishia wananchi huduma za Kinga, Tiba na Elimu ya Afya mahali walipo bila vikwazo.
Rais Dkt. Samia ameeeleza kuwa,Tanzania iko katika mchakato wa kutimiza lengo la kufikisha huduma za afya kwa watu wote (UHC), dira inayotekelezwa tangu kupitishwa kwa Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote wa mwaka 2023.
Kuhusu ugonjwa wa Marburg, Rais Dkt. Samia amesema, kufuatia tetesi za uwepo wa ugonjwahuo mkoani Kagera, Serikali ilichukua hatua za kuwafanyia uchunguzi watu waliodhaniwa kuwa na virusi vya ugonjwa huo kwa kushirikiana na wataalamu wa afya katika maeneo hayona Januari 11,2025 ikatuma timu maalumu ya dharura.
Sampuli za vipimo vya waliodhaniwa kuwa na virusi vya ugonjwa zilichukuliwa na kupimwa na kubaini kuwa mtu mmoja ndiye aliyekuwa na virusi hivyo huku wengine wakigundulika kuwa na magonjwa mengine.
Hii ni mara ya pili kutokea kwa virusi vya Marburg nchini Tanzania ambapo kwa mara ya kwanza mlipuko wa virusi hivyo ulitokea mwezi Machi mwaka 2023 mkoani Kagera.
Rais Dkt. Samia ameongeza kuwa,Tanzania iko salama na inawakaribisha kufanya shughuli zakibiashara pamoja na shughuli zingine.
Kwa upande wake Dkt. Tedros amesema WHO itaendelea kuiunga mkono Tanzania katika kukabiliana na kudhibiti mlipuko wa virusi hivyo.
Dkt. Tedros amesema jitihada za Serikali katika kukabiliana na mlipuko uliotokea mwaka 2023 zimeijengea uwezo ambao unaiwezesha Tanzania kuudhibiti kwa uharaka mlipuko uliotokea hivi sasa.
Aidha,Dkt.Tedros amempongeza Rais Dkt. Samia kwa kujidhatiti kwake katika huduma ya afya kwa wote kupitia kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023.