NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa, thamani ya shilingi inatarajiwa kuwa imara katika robo ya kwanza ya mwaka 2025.
Ni kutokana na kuwepo kwa ukwasi wa kutosha wa fedha za kigeni uliopatikana katika robo ya nne ya mwaka 2024.
Vilevile utekelezaji wa sera ya fedha kutokana na uamuzi wa kubakiza Riba ya Benki Kuu kuwa asilimia 6, na bei za bidhaa katika soko la dunia kuwa nafuu.
Gavana wa BoT ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ameyasema hayo leo Januari 8,2025 katika ofisi za makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam mbele ya wanahabari na wadau mbalimbali wa Sekta ya Fedha nchini.
Katika kikao hicho, Gavana Tutuba alikuwa akitoa taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya Benki Kuu ya Tanzania ambayo ilifanya kikao chake cha kila robo mwaka Januari 7,2025 na kufanya tathmini ya mwenendo wa hali ya uchumi wa dunia na hapa nchini.
Gavana Tutuba amesema, uimara huo wa shilingi vilevile, utachangiwa na Benki Kuu kuendelea kusimamia utekelezaji wa Kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu kinachohimiza matumizi ya shilingi katika kufanya miamala hapa nchini ili kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni yasiyokuwa ya lazima.
"Aidha, Benki Kuu inatarajia kuendelea kuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni,na kuongeza fedha za kigeni pale itapohitajikata."
Pia, amesema akiba iliyopo sasa ni zaidi ya dola za Marekani bilioni 5.5, kiwango ambacho kinatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa zaidi ya miezi 4.7.
"Akiba hiyo inatarajiwa kubaki katika kiwango hicho katika robo ya kwanza ya mwaka 2025 kutokana na juhudi zinazofanywa na Benki kuu katika kuongeza akiba ya fedha za kigeni, ikiwemo kununua dhahabu hapa nchini."