DAR-Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi Utabiri wa Msimu wa Mvua za Masika 2025 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka.
Akizungumza wakati wa mkutano na vyombo vya habari katika ukumbi wa mikutano wa Ubungo Plaza leo Januari 23,2025, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Mwakilishi wa Kudumu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Changa amesema mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki.
Sambamba na Mashariki mwa mikoa ya Mara na Simiyu huku mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zikitarajiwa katika maeneo ya Pwani ya Kaskazini, Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma na Ukanda wa Ziwa Victoria.
“Mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki pamoja na Mashariki mwa Mikoa ya Mara na Simiyu.
"Aidha, mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zinatarajiwa katika maeneo ya Pwani ya Kaskazini, Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma na Ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga na magharibi mwa mikoa ya Simiyu na Mara) katika kipindi cha Msimu wa Masika, 2025.”
Vilevile, taarifa hiyo imeelezea pia ongezeko la mvua linatarajiwa katika kipindi cha mwezi Aprili sambamba na kutoa angalizo la matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo vipindi vya mvua kubwa kujitokeza hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani.
Akizungumzia athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Chang’a alisema Mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zinazotarajiwa katika baadhi ya maeneo zinaweza kupelekea upungufu wa upatikanaji wa maji kwa matumizi ya majumbani, kilimo na ufugaji.
Tags
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Msimu wa Masika
Tanzania Meteorological Agency (TMA)