DODOMA-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akiambatana na Mwenza wake Mama Mbonimpaye Mpango wameungana na Waumini mbalimbali katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Mwaka Mpya 2025 iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska Kiwanja cha Ndege mkoani Dodoma.
Akizungumza na waumini mara baada ya Misa hiyo, Makamu wa Rais ameungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali kuwatakia watanzania wote heri na baraka kwa mwaka mpya 2025.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa viongozi wa dini, waumini na watanzania kwa ujumla kuliombea Taifa kuwa na amani hususani katika kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka huu.
Amesema, ni muhimu kuliombea Taifa ili kupata viongozi wenye hofu ya Mungu, viongozi waadilifu na wanaojali haki za wanyonge.
Ameongeza kwamba kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha Taifa linakuwa na amani.
Aidha,Makamu wa Rais amewahimiza waumini kuiombea dunia amani kutokana na machafuko yanayoendelea katika maeneo mbalimbali.
Pia amesisitiza kuwaombea watanzania wenye wenye matatizo mbalimbali ili waondokane na changamoto hizo.