DAR-Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, Tundu Lissu ameshinda nafasi ya uenyekiti wa chama hicho Taifa.
Ushindi wa Lissu unakuja baada ya kumuangusha mpinzani wake aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho kwa miaka zaidi ya 20,Freeman Mbowe.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Januari 21,2025 katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Tundu Lissu amepata kura 513 sawa na asilimia 51.5.
Aidha,Freeman Mbowe amepata kura 482 sawa na asilimia 48.3 na Odero Charles Odero yeye amepata kura moja sawa na asilimia 0.01.
Mbali na hayo,Freeman Mbowe ambaye alikuwa anatetea nafasi yake kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X ameandika ujumbe wa kukubali kushindwa.
"Nimepokea kwa mikono miwili maamuzi ya Uchaguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama chetu CHADEMA uliohitimishwa leo asubuhi 22 Januari 2025. Nampongeza Mhe. Tundu Lissu na wenzake kwa kuaminiwa kutwikwa jukumu la Uongozi wa Chama."
Mbowe ameikiongoza CHADEMA tangu alipochaguliwa nafasi hiyo mwaka 2004 akirithi mikoba ya Bob Makani aliyeongoza chama hicho kuanzia mwaka 1999.