ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewasisitiza viongozi wa dini,wanasiasa na waandishi wa habari kutumia majukwaa yao kutoa kauli nzuri zenye kuleta umoja ndani ya jamii na amani ya nchi.
Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipojumuika na waumini wa dini ya Kiislamu katika Sala ya Ijumaa iliyofanyika Msikiti Mkuu wa Ijumaa, Malindi Mkoa wa Mjini Magharibi.
Alhaj Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa,viongozi wa dini na wanasiasa wawe na kauli zenye kusikilizwa na watu wengi hivyo ni vema wakatumia majukwaa yao kutoa kauli njema zitakazojenga Umoja,Undugu, Mshikamano na Amani.
Akiwazungumzia waandishi wa habari,Alhaj Dkt.Mwinyi amewahimiza kutumia kalamu zao vizuri na kujihadhari na yale wanayoyaandika katika Televisheni,Redio na Mitandao ya Kijami kuwa hayana viashiria vya uvunjifu wa amani.
Halikadhalika, Alhaj Dkt.Mwinyi amefahamisha kuwa kwa miaka ningi iliyopita uzoefu umeonesha kuwa, Zanzibar ilikuwa ikiingia katika mifarakano kila unapofika wakati wa uchaguzi jambo lisilopaswa kutokea tena.Aidha,Alhaj Dkt.Mwinyi amesema,ni lazima nchi ioneshe kuwa inaweza kufanya uchaguzi kwa amani,hatimaye ipige hatua zaidi za maendeleo.