DAR-Mwenendo wa uchumi wa Tanzania Bara na Zanzibar umeendelea kuwa imara mwaka 2024 na mfumuko wa bei umeendelea kuwa tulivu katika kipindi chote cha mwaka 2024, ukiwa chini ya lengo la asilimia 5 kwa Tanzania Bara kwa wastani wa asilimia 3 na kwa Zanzibar mfumuko wa bei ulipungua hadi asilimia 4.5 mwezi Novemba 2024.
“Mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kuwa tulivu katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, ukibakia katika viwango vya kati ya asilimia 3.1 na asilimia 4 kutokana na kuendelea kuwepo kwa chakula cha kutosha, utulivu wa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni, umeme wa uhakika, na kushuka kwa bei za bidhaa katika soko la dunia, yakiwemo mafuta ghafi," amesema Gavana Emmanuel Tutuba.
Akitoa taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu mbele ya wakuu wa benki na taasisi za fedha na waandishi wa habari, tarehe 8 Januari 2025, Gavana Tutuba amesema ukuaji wa ujazi wa fedha na mikopo kwa sekta binafsi uliendelea kuwa wa kasi ya kuridhisha mwaka 2024, ambapo ulifikia wastani wa asilimia 12.5 na asilimia 16.9.
Ukwasi wa fedha za kigeni uliongezeka kwa kiwango kikubwa katika robo ya nne ya mwaka 2024. Hali hii inatokana na kuimarika kwa mazingira ya upatikanaji fedha duniani kutokana na kupungua kwa riba katika nchi zinazoendelea na kuongezeka kwa mapato ya fedha za kigeni nchini kutokana na shughuli za utalii, mauzo ya dhahabu, korosho na tumbaku.
“Utekelezaji wa sera ya fedha uliolenga kupunguza athari za kushuka kwa thamani ya shilingi kwenye mfumuko wa bei ulichangia kuiimarisha shilingi,” amesema Gavana Tutuba.
Ameongeza kuwa kutokana na kuimarika kwa ukwasi wa fedha za kigeni nchini, shilingi iliimarika dhidi ya fedha za kigeni, soko la fedha za kigeni lisilo rasmi lilitoweka, na matarajio kuwa thamani ya shilingi itaendelea kushuka yalififia, hali ambayo imekuwa na manufaa ya kuwa na mfumuko wa bei mdogo, na kupunguza gharama ya kulipa madeni nje ya nchi.
Thamani ya shilingi inatarajiwa kuwa imara katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, kutokana na kuwepo kwa ukwasi wa kutosha wa fedha za kigeni uliopatikana katika robo ya nne ya mwaka 2024 kutokana na utekelezaji wa sera ya fedha na bei za bidhaa katika soko la dunia kuwa nafuu.
Aidha, Benki Kuu imeendelea kusimamia utekelezaji wa Kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu kinachohimiza matumizi ya shilingi katika kufanya miamala hapa nchini na hivyo kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni yasiyokuwa ya lazima.
Meneja Uhusiano wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),Vicky Msina akiongoza kikao hicho na kumkaribisha Gavana Tutuba aweze kuwasilisha taarifa ya MPC.
Benki Kuu inatarajia kuendelea kuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni. Akiba iliyopo ni zaidi ya dola za Marekani bilioni 5.5, kiwango ambacho kinatosheleza zaidi uagizaji wa bidhaa na huduma kwa zaidi ya miezi 4.7.
Akiba hiyo inatarajiwa kubaki katika kiwango hicho katika robo ya kwanza ya mwaka 2025 kutokana na juhudi zinazofanywa na Benki Kuu katika kuongeza akiba ya fedha za kigeni, ikiwemo kununua dhahabu hapa nchini.
Utekelezaji wa sera ya bajeti ulikuwa wa kuridhisha, ambapo makusanyo ya mapato yatokanayo na kodi yalivuka malengo, kutokana na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi, maboresho katika usimamizi wa kodi na utayari wa wananchi kulipa kodi na Serikali kuendelea kufanya matumizi kuendana na rasilimali zilizopo.
Deni la Taifa liliendelea kuwa himilivu, ambapo kwa mwaka 2023/24 lilikuwa takriban asilimia 41.1 ya Pato la Taifa (GDP) kwa thamani halisi ya sasa (NPV). Kiwango hiki kilikua chini ya ukomo wa uhimilivu wa nchi na kigezo cha mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) cha asilimia 55 na asilimia 50, mtawalia.
Kwa kuzingatia thamani ya bei za sasa, deni la Taifa lilikuwa asilimia 46.1 ya Pato la Taifa, chini ya kigezo cha mtangamano kwa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) cha ukomo wa asilimia 60.
Sekta ya nje imeendelea kuimarika zaidi katika mwaka 2024. Nakisi ya urari wa malipo ya nje (current account deficit) ilipungua kufikia asilimia 2.7 ya Pato la Taifa, ikiwa ni nakisi ya chini kabisa katika kipindi cha miaka minne iliyopita, ikilingashwa na asilimia 3.7 mwaka 2023.
Mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi yalifikia asilimia 20 ya Pato la Taifa kutoka asilimia 18 katika mwaka 2023, kutokana na ongezeko la shughuli za utalii, mauzo ya dhahabu, korosho na tumbaku nje ya nchi. Uagizaji wa bidhaa na huduma toka nje ya nchi ulikuwa asilimia 21 ya Pato la Taifa ukilinganishwa na asilimia 20.3 mwaka 2023.
Katika robo ya nne ya mwaka 2024, urari wa malipo ya kawaida ulikadiriwa kufikia nakisi ya dola za Marekani milioni 643.4, ikiwa ni takriban nusu ya nakisi iliyorekodiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2023.
Kwa upande wa Zanzibar, urari wa malipo ya kawaida unakadiriwa kuwa na ziada ya dola za Marekani milioni 124.5, ikilinganishwa na ziada ya dola za Marekani milioni 136.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2023, kutokana na ongezeko la uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi.
Sekta ya nje inatarajiwa kuendelea kuimarika mwaka 2025, ambapo nakisi ya urari wa malipo ya kawaida kwa Tanzania Bara inatarajiwa kupungua hadi asilimia 2.4 ya Pato la Taifa.
“Benki Kuu itaendelea kuhakikisha uwepo wa ukwasi unaoendana na mahitaji ya uchumi, ili kufikia malengo ya kuwa na mfumuko wa bei mdogo na kuchagiza ukuaji wa shughuli za uchumi. Katika kufikia malengo haya, Benki Kuu itaendelea kufuatilia mwenendo wa uchumi na kuchukua hatua stahiki pale itakapohitajika,” amesema Gavana ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Sera ya Fedha.