MOROGORO-Uongozi wa Chama cha Wafanyakazi (TUGHE) tawi la Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) umepongezwa kwa kusimamia vyema maslahi ya wafanyakazi, hali iliyosaidia kupunguza malalamiko yao kwa kiwango kikubwa.
Pongezi hizo zimetolewa na Meneja wa Utawala na Rasilimali Watu wa TFRA, Naomi Fwemula, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi, Victoria Elangwa wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa mamlaka hiyo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Morena, Morogoro.
"TUGHE imesaidia sana katika kusimamia haki za wafanyakazi na kuishauri menejimenti kuhusu mbinu bora za kutatua changamoto za watumishi,"amesema Fwemula.

Kamishna Msaidizi wa Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Andrew Mwalwisi, aliwaasa watumishi hao kuheshimu sheria, kanuni, na miongozo ya utumishi wa umma ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima eneo la kazi.
Katika mada yake kuhusu Haki na Wajibu wa Watumishi wa Umma, Mwalwisi alisisitiza kuwa kanuni za utumishi ndizo zinazoeleza haki za mtumishi, hivyo ni jukumu la kila mfanyakazi kuzizingatia ili kuepuka mgongano na waajiri wao.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi (TUGHE) TFRA, Aziz Mtambo, amewasihi watumishi wa Mamlaka kujiunga na chama cha wafanyakazi ili waweze kunufaika na huduma zinazotolewa na chama hicho lakini pia itasaidia uundaji wa Mkataba wa Hali bora utakosaidia kusimamia maslahi ya wafanyakazi.
Alibainisha kuwa, kwa sasa ni watumishi 34 pekee kati ya 89 wa TFRA waliojiunga na TUGHE, lakini idadi hiyo imeongezeka kutoka 12 waliokuwepo mwaka wa 2021/2022.
Tags
Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE)
Habari
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania
TFRA
TFRA Tanzania
TUGHE Tanzania