ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amefahamisha kuwa, dhamira ya kuwakodisha wawekezaji Visiwa hivyo ni kuviendeleza kwa uwekezaji ili nchi inufaike navyo na kuinua uchumi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipozungumza na wananchi katika ufunguzi wa Hoteli ya BAWE ISLAND COCOON COLLECTION iliyopo katika Kisiwa cha Bawe. Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha,Rais Dkt.Mwinyi ametoa muda wa miezi mitatu kwa wawekezaji waliokodishwa visiwa vidogo vidogo na kushindwa kuanza uwekezaji kuwa watanyang'anywa ifikapo muda huo.
Rais Dkt.Mwinyi akizungumzia ufunguzi wa Hoteli ya Bawe ameeleza kuwa, Serikali imefanikiwa kwa kuitekeleza asilimia kubwa Ilani ya CCM hususani katika utalii kwani vyumba zaidi ya 15,132 vya hoteli vimejengwa na kuvuka lengo la ilani la vyumba 10,000 kilichoainishwa katika Ilani 2020-2025.
Akizungumzia suala la ajira amewahimiza vijana kujitahidi kusoma kwa bidii ili kuwa na weledi wa kuajirika katika Sekta ya Hoteli na Utalii kwa ujumla.
Halikadhalika, Rais Dkt.Mwinyi ameipongeza Menejimenti ya Hoteli ya Bawe kwa kutekeleza Mkataba wa Uwekezaji katika miradi mitatu Tofauti Ikiwemo Prison Island, Hoteli ya Gold Star Nungwi na huo wa Bawe.
Naye Rais wa Jamhuri ya Miungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza baada ya kuifungua hoteli hiyo ameeleza kuwa, uamuzi wa Serikali wa kuvikodisha visiwa una manufaa makubwa kwa Zanzibar kwani mbali na wawekezaji hao kulipa kodi na kuongeza mapato ya nchi pia utaitangaza nchi Kimataifa.
Hoteli hiyo imegharimu kiasi cha dola za kimarekani milioni 42 hadi kukamilika kwake ina vyumba 400.