NA GODFREY NNKO
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Kassim Majaliwa amesema,katika kipindi cha Novemba, 2020 hadi Novemba, 2024 Serikali imetekeleza mikakati iliyolenga kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.
Vilevile kuboresha vyama vya ushirika, miundombinu ya umwagiliaji na upatikanaji wa pembejeo.
Ameyasema hayo Januari 19,2025 jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi Desemba,2024.
Ni mbele ya wajumbe ya wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM ambao umeongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Majaliwa amesema, mafanikio makubwa ni pamoja Serikali kuimarisha Mfumo wa Stakabadhi Ghalani, ambapo vyama vya ushirika vimeongezeka kutoka 2,150 mwaka 2020 hadi 4,060 mwaka 2024.
Amesema,mazao yaliyouzwa ni pamoja na choroko, dengu, mpunga, mbaazi, kahawa, korosho na pamba.
"Serikali imechagiza mchakato wa kuanzisha Benki ya Ushirika, ambayo iko katika hatua za mwisho, ikiwemo kufikia lengo la ukwasi wa shilingi bilioni 50."
Amesema kuwa, pia kuna ongezeko la wanachama wa vyama vya ushirika kwa asilimia 42.4 kutoka vyama milioni 5.9 mwaka 2020 hadi milioni 8.4 mwaka 2024.
Jambo lingine ni kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula kutoka tani milioni 18.6 mwaka 2020 hadi tani milioni 22.8 mwaka 2024.
Majaliwa amesema,uzalishaji huo ulichagizwa na kuogezeka kwa upatikanaji wa mbolea kwa asilimia 107 kutoka tani 586,604 mwaka 2020 hadi tani 1,213,729 mwaka 2024;
Pia, amesema kuna ongezeko katika ujenzi wa miundombinu ya eneo la umwagiliaji kutoka hekta 561,383 mwaka 2020 hadi hekta 983,466 sawa na asilimia 82 ya lengo la Ilani ya Uchaguzi ya CCM la kufikia hekta milioni 1.2.
"Ongezeko hilo limetokana na kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa skimu mbalimbali za umwagiliaji zikiwemo skimu mpya 34 zenye jumla ya hekta 31,773 ikijumuisha skimu ndogo 11 (hekta 2,481), skimu za kati 16 (hekta 13,520) na skimu kubwa 7 (hekta 15,772).
"Aidha, kujenga skimu mpya 35 zenye jumla ya hekta 60,896 ikijumuisha skimu ndogo 9 (hekta 1,862), skimu za kati 15 (hekta 14,534) na skimu kubwa 11 (hekta 44,500)."
Amesema,pia Serikali imejenga mabwawa mapya 19 yenye uwezo wa zaidi ya mita za ujazo milioni 131.53 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.
Mbali na hayo,Serikali imejenga maghala 42 yenye uwezo wa kuhifadhi tani 49,000 za mazao na vihenge vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 190,000 za mazao na hivyo kuchangia juhudi za Serikali za kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno.
Waziri Mkuu amesema, mafanikio mengine ni kufunguliwa kwa masoko mapya 10 ya kilimo kwa mazao kama vile vanila, karafuu, pilipili manga, nanasi, kakao, tumbaku, ndizi na parachichi, katika nchi za China, India, Canada, Marekani, Israeli, Malaysia, Indonesia, Singapore, Uturuki, Zambia na Afrika Kusini;
"Vituo 45 vyenye matrekta 500 vilianzishwa katika mikoa 15 ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija.
"Aidha, vijana zaidi ya 193,000 waliwezeshwa kupata ekari 491,929 kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na mbegu bora 46 zimegunduliwa na kuidhinishwa na Kamati ya Kitaifa ya Mbegu ikiwemo za mtama, viazi vitamu na karanga."
Waziri Mkuu ameongeza kuwa, aina 11 za mbegu na miche bora ya chikichi, migomba, mihogo, minazi na pareto zimegunduliwa na mafunzo kuhusu matumizi ya mbegu bora yametolewa kwa wadau 2,034,859 nchini.