DAR-Timu ya Wataalamu kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDCP) imetoa mafunzo kwa waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam ili kujenga uelewa kwa waandishi hao na jamii kwa ujumla.
Kaimu Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDCP),Dkt. Faraja Lyamuya akiwasilisha mada kuhusu ugonjwa wa Matende na Mabusha kwa waandishi wa habari Jumanne Januari 21,2025 jijini Dar es Salaam.
Mafunzo hayo ni hatua muhimu ya utoaji elimu kwa umma kuhusu magonjwa Matano yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ambayo ni Ugonjwa wa Matende na Mabusha, Trakoma, Usubi, Minyoo ya Tumbo pamoja na Kichocho.
Wizara ya Afya kupitia Mpangho wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele imetoa elimu hiyo kwa waandishi ikiwa ni hatua muhimu ya maandalizi yake kuelekea maadhimisho ya Siku ya Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele Duniani.
Kaimu Meneja wa Mpango huo Nchini Dkt. Faraja Lyamuya akifungua semina hiyo kwa waandishi hao leo January 21, 2025 Jijini Dar es Salaam amesema Halmashauri 114 nchini zimeacha kugawa kingatiba za ugonjwa wa matende na mabusha kutokana na mafanikio ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo ambao umepungua na kufikia chini ya asilimia mbili.
Aidha Dkt Lyamuya amezitaja Halmashauri hizo kuwa ni halmashauri za Manispaa ya Kinondoni na Lindi, Halmashauri za Wilaya ya Mtama, Pangani na Mtwara Mikindani.
Katika hatua nyingine Dk. Lyamuya ameeleza kuwa, imani potofu zilizopo katika jamii zinafifisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo akizitaja Imani izo kuwa ni pamoja na baadhi ya watu kuamini kwamba ugonjwa wa matende na mabusha ni wa urithi, unatokana na kulogwa na kuamini ni ugonjwa unaothiri ukanda wa Pwani pekee.
"Sio kweli kwamba ugonjwa wa matende na mabusha au ngiri maji, huambukizwa kwa kunywa maji ya madafu, wala si ugonjwa wa kulogwa, sio kweli kwamba ni ugonjwa unaothiri ukanda wa Pwani pekee bali maeneo yote yenye mbu wenye vimelea watu wanaweza kupatwa na huu ugonjwa.
Naye Afisa Mpango, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDCP) Dk. Lilian Ryatura amesema, Halmashauri zilizokuwa na maambukizi ya juu ya zaidi ya asilimia 5 ya ugonjwa wa Trachoma (vikope) zilikuwa ni halmashauri 69 lakini baada ya kutoa kingatiba aina ya Zithromax, zimepungua hadi kufikia halmashauri tisa pekee.
Amezitaja halmashauri hizo kuwa ni, Longido, Ngorongoro, Monduli, Kiteto, Simanjiro, Kalambo, Mpwapwa, Kongwa na Chamwino huku akisisitiza kuwa ugonjwa huo hutibika kwa mtu kufanyiwa upasuaji mdogo wa kusawazisha kope.
Kwa upande wa ugonjwa Kichocho ambao ni miongoni mwa magonjwa ambayo yalikuwa hayapewi kipaumbele, Afisa Mpango Dk. Mohamed Nyati ameiasa jamii kumeza kingatiba ya Kichocho kila zinazotolewa kwenye jamii na shuleni kama njia kujikinga na ugonjwa huo.
Ameizitaja njia nyingine za kujikinga na ugonjwa huo kuwa ni pamoja na kutumia choo kwa haja kubwa na ndogo, kuepuka kufua, kuogelea, au kuosha vyombo ndani ya maji yaliyotuama kama mabwawa, madimbwi na ziwani.
Ruth Mchomvu ni Afisa Mpango, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDCP) amesema, watu zaidi ya watu milioni 7.2 wanaoishi katika mikoa ya Morogoro, Ruvuma, Mbeya, Songwe, Tanga, Iringa, Njombe, Iringa na Dodoma wako hatarini kupata ugonjwa wa Usubi, ugonjwa ambao unaweza kutibika na kuzuilika.
Lakini katika kuzuia hatari ya kupata ugonjwa huo, Mchomvu amesema ni muhimu kwa wananchi kumeza kingatiba za ugonjwa huo kila zinapotolewa kwenye jamii kwa kuwa dalili za ugonjwa huo huwa hazijtokezi mapema.
Sehemu ya Waandishi wa Habari walioshiriki Mafunzo ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDCP) wakifuatilia kwa makini mada kuhusu ugonjwa wa Matende na leo Jumanne Januari 21,2025 jijini Dar es Salaam.
Kuhusu ugonjwa wa minyoo ya tumbo, Afisa Mpango Catherine Mahimbo amewaeleza waandishi wa habari kuwa, ugonjwa huo unaathiri watu wa rika zote wakiwemo watu wazima katika jamii na usipotibika mapema husababisha madhara lukuki.
Mahambo ameyataja baadhi ya madhara kuwa ni pamoja na kupungua kwa damu, utapiamlo, kupungua uzito.
Madhara mengine ni udumavu wa akili na mwili kwa watoto, utumbo kujiunga, kujiziba na hatimaye kupasuka.
Mafunzo ya leo kwa waandishi wa habari ni sehemu ya mfululizo wa matukio kuelekea maadhimisho ya Siku ya Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele Duniani ambayo huadhimishwa kila tarehe 30 ya Mwezi Januari ambapo kulia mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu inasema "Tuungane. Tuchuke hatua. Tutokomeze Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele".