Walimu 201,707 kufanyiwa usaili kujaza nafasi 14,648

DODOMA-Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema,walimu
201,707 wanatarajiwa kufanyiwa usaili kuanzia Januari 14 hadi Februari 24, mwaka huu.

Ni kwa ajili ya kujaza nafasi 14,648 zilizotangazwa na serikali ili kupunguza uhaba wa watumishi wa kada hiyo nchini.
Simbachawene ameyasema hayo Januari 11,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu usaili huo jijini Dodoma.

Amesema,kuanzia Januari 14 hadi Februari 24, 2025, usaili wa kada za ualimu utaendeshwa na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais (UTUMISHI).

Vilevile utahusisha Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Afya, Tume ya Utumishi wa Walimu.


Sambamba na Ofisi za Wakuu wa Mikoa yote na wataalamu mbalimbali kutoka katika Taasisi za Umma.

“Ninapenda kuchukua nafasi hii kuwasihi sana wale wote walioitwa kwenye usaili wajiandae vyema kwa usaili huo kwani nafasi hizi ni za ushindani.

“Vilevile, kulingana na mahitaji yetu ya elimu kwa sasa, tutaajiri wataalamu wa fani za Amali. Hivyo, nawasihi sana wale wote watakaopata nafasi ya kuajiriwa, wawe tayari kujiendeleza ili kuweza kukidhi matakwa ya ajira zao katika Utumishi wa Umma."

Waziri huyo amesema, usaili huo wa kada za ualimu utafanyika katika mkoa ambao kila msailiwa anaishi lengo ni kuwapunguzia gharama za kusafiri na mambo mengine.

Amesema,Sekretarieti ya Ajira ilitoa matangazo kumtaka kila msailiwa kuhuisha taarifa zake katika akaunti yake ya Ajira Portal sehemu iliyoandikwa current physical adress kwani ndipo wamewapangia vituo vya usaili kulingana na anuani walizojaza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news