Wananchi Kilimanjaro wapongeza huduma ya Kliniki ya Sheria bila malipo

KILIMANJARO-Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeendelea kusogeza huduma karibu kwa Wananchi kupitia Kliniki ya Sheria bila malipo kwa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro.Kliniki hiyo ilianza tarehe 21 Januari 2025 na kufikia kilele chake tarehe 27 Januari 2025 katika viwanja vya Stendi ya Vumbi jirani na Stend kuu ya Mabasi ya Moshi.

Akizungumza wakati wa kilele cha Kliniki ya Sheria bila malipo kwa Wananchi wa Kilimanjaro, Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi. Tamari Mndeme amesema Ofisi hiyo inajivunia kuendesha Kliniki hiyo ambapo imeweza kuwafikia wananchi wenye changamoto mbalimbali za kisheri.
"Kliniki hii imefanyika kwa mafanikio makubwa na tumeweza kuwahudumia wananchi kama ambavyo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilikuwa inakusudia". Amsema Bi. Tamari

Aidha,Bi.Tamari ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa Ushirikiano walioutoa kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kuhakikisha Kliniki ya Sheria bila malipo inafanyika kwa ufanisi mkubwa.

"Nachukua nafasi hii kuushukuru uongozi wa mkoa wa Kilimanjaro ukiongozwa na Mhe. Nurdin Babu Mkuu wa Mkoa kwa ushirikiano waliotupatia na pia kuhamasisha wananchi kujitokeza kuja kupata huduma kwenye kliniki hii, tunawashukuru sana,"ameeleza Bi.Tamari.

Katika hatua nyingine, Bi. Tamari Mndeme amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Kamati ya Mkoa ya Ushauri itaendelea kutoa huduma za kisheria kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kilimanjaro hususani Vijijini.

Kwa upande wake Katibu Kamati ya Ushauri wa Kisheria ya mkoa wa Kilimanjaro, Bi. Kissa Lyimo ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kufanya Kliniki ya Sheria bila malipo kwa wanachi wa mkoa wa Kilimanjaro kwa kuwa kliniki hiyo imeweza kusikiliza na kutoa ushauri kwa wananchi wengi wa mkoa huo.
"Tunawashukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuja kuwahudumia wananchi wa mkoa wetu kwani kupitia kliniki hii wananchi wameweza kusaidiwa na kutatuliwa changamoto za kisheria,"amesema Bi. Lyimo.

Bw. Hamisi Bakari mmoja ya wananchi waliojitokeza na kupata huduma katika Kiniki ya Sheria bila malipo ameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuwafikia watu wengi ambao hawana uwezo wa kulipia huduma za sheria, huku akiomba kliniki hiyo ifanyike mara kwa mara ili iweze kutatua migogoro ya Ardhi ambayo imekuwa mingi kwa mkoa wa Kilimanjaro.

"Napenda kutoa shukrani zangu kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutoa huduma hii bure ambapo tumeweza kueleza matatizo yetu na kuhudumiwa, nawaomba kliniki hii iendelee kwa mkoa wa Kilimanjaro ambapo matatizo ya ardhi yamekuwa mengi sana,"amesema Bw.Bakari.

Nae Bi. Khadia Kimaro amefurahishwa na huduma alizozipata katika kliniki hiyo huku akipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutoa Ushauri wa Kisheria bila malipo, pia ameomba kliniki hiyo iongozwe muda ili iweze kuhudumia wananchi wengi zaidi.
"Nimepokelewa vizuri na Mawakili wamenihudumia kwa haraka, Kliniki hii imekuwa msaada mkubwa kwetu sisi ambao hatuna uwezo wa kuwalipa Wanasheria, ningeomba pia waongeze muda siku ziwe nyingi za kutoa huduma naamini watasaidia watu wengi sana,"amesema Bi.Khadija.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news