DAR-Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Hamis Mwinjuma ameongoza hafla muhimu ya kusaini Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) kati ya Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).
Hafla hiyo, iliyofanyika leo, Januari 13, 2025, katika ukumbi wa mikutano wa makao makuu ya TAA, inalenga kuhakikisha kuwa wasanii wa Kitanzania wananufaika na mirabaha kutokana na matumizi ya kazi zao za muziki katika viwanja vya ndege nchini.
Makubaliano haya yanahimiza matumizi ya kazi za muziki wa Kitanzania katika maeneo yote ya TAA, ambapo asilimia 80% ya nyimbo zitakazopigwa zitakuwa za wasanii wa ndani, huku asilimia 20% pekee zikiwa za kimataifa.
Mpango huu unaonyesha dhamira ya dhati ya COSOTA na TAA katika kukuza kipato cha wasanii wa ndani na kuchochea ukuaji wa sekta ya sanaa na burudani nchini.
Aidha, TAA imejipambanua kama taasisi ya mfano kwa kuwa ya kwanza miongoni mwa taasisi chini ya Wizara ya Uchukuzi kutekeleza mpango huu wa kimkakati.
Kupitia makubaliano haya, TAA inaweka msingi wa kuimarisha matumizi ya kazi za muziki wa Kitanzania, hatua inayotazamiwa sio tu kuwaongezea wasanii kipato, bali pia kuwapa nafasi ya kufikia hadhira kubwa zaidi ndani na nje ya nchi.
Katika hotuba yake, Mheshimiwa Mwinjuma amepongeza juhudi za COSOTA na TAA katika kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan la kuimarisha sekta ya sanaa na muziki kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Amesisitiza kuwa makubaliano haya yanafungua njia ya kuimarisha usimamizi wa hakimiliki za wasanii na kutoa wito kwa taasisi nyingine za umma na binafsi kuiga mfano huu.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa COSOTA, TAA, BASATA, BODI YA FILAMU na waandishi wa habari, na wadau mbalimbali wa sekta ya sanaa, uchukuzi, na burudani. Mwisho wa hafla hiyo, Naibu Waziri alitoa shukrani kwa wote walioshiriki katika kufanikisha hatua hii kubwa ambayo inaleta matumaini makubwa kwa wasanii wa Kitanzania.