DODOMA-Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Methusela Ntonda amewaasa Watumishi wapya Serikalini kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma kwa kuonesha tabia njema na kuwa mfano wa kuigwa mahali pa kazi na kwenye jamii inayowazunguka.
Ntonda ametoa wito huo Januari 8, 2024 wakati akifungua mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wapya wa Umma katika ukumbi wa wizara hiyo uliopo jijini Dodoma.
Akiwapongeza watumishi hao wapya kwa kupata ajira Serikalini,Methusela amewataka watumishi hao kufahamu haki na wajibu wao kama watumishi wa Umma, kutambua majukumu yao pia kutoshiriki vitendo vya uvunjifu wa amani kwani wao ni kioo cha jamii wanayoishi sambamba na kutunza siri za Serikali.
Wakati huohuo, Mkurugenzi wa Utawala na usimamizi wa rasilimali watu, Bi. Savera Kazaura amewataka watumishi hao kuwa watoa huduma bora kwa kutoa huduma kwa Umma kwa wakati na ufanisi pamoja na kusisitiza matumizi bora ya mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na kusoma vitu vyenye kujenga taaluma zao.