Watumishi wa umma watakiwa kufanya mazoezi

NA RESPICE SWETU

WATUMISHI wa umma katika wilaya ya Kasulu, wametakiwa kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kuiweka miili yao katika afya njema.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Issac Mwakisu alipokuwa akifungua bonanza la michezo la watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu lililofanyika mwishoni mwa wiki katika viwanja vya chuo cha Ualimu cha Kasulu.
Amesema utamaduni wa kuandaa bonanza la michezo kama hilo unastahili kuigwa na kwamba, michezo hiyo isisubiri kufanyika mara moja tu kwa mwaka.

Mwakisu ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya usalama ya wilaya ameongeza kuwa, watumishi wanapokutana na kushiriki katika michezo, huongeza mahusiano baina yao na kuimarisha usalama wa eneo lao.

“Tukicheza pamoja leo hautanidhuru kesho, michezo ni afya na michezo ni usalama, nampongeza sana mkurugenzi mtendaji wa halmashauriya wilaya ya Kasulu kwa ubunifu huu,” amesema Mwakisu.
Awali akimkaribisha mkuu wa wilaya ya Kasulu kufungua bonanza hilo, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu Dkt. Semistatus Mashimba amesema, bonanza hilo limefanyika kwa lengo la kuukaribisha mwaka mpya wa 2025 na kuuaga mwaka 2024.

Bonanza hilo lilihusisha mpira wa pete, riadha, karata, kukimbiza kuku, kuvuta kamba na kukimbia kwenye magunia ambapo zawadi mbalimbali zilitolewa kwa washindi wa michezo hiyo huku ushindi wa jumla ukienda kwa watumishi wa makao makuu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news