DAR (Januari 6,2025)-Waandaa maudhui ya mtandaoni (content creators) ni kundi muhimu ambalo, kazi zake zikizingatia weledi na miongozo ya kisera na sheria, hakika lina mchango chanya kwenye maendeleo na ustawi wa jamii sekta zote.
Hata hivyo, kumeibuka wimbi kubwa la waandaa maudhui mtandaoni ambalo linafanya kazi zake bila weledi wa aina yoyote, jambo lenye athari kubwa kwa maendeleo na ustawi wa jamii.
Mathalani kwa uchache kabisa, hivi karibuni kaonekana mmoja akisambaza maudhui ya kuuza figo za mtoto, kuna mwingine anarusha maudhui ya kuandaa vinywaji na vyakula vichafu na kujitapa anawauzia wananchi wa Kariakoo na wengine wengi.
Kuna wale wengine wanasambaza maudhui ya kufanya mapenzi hadharani yakiwemo ya jinsia moja, wengine wanasambaza maudhui kuhusu fursa za kujipatia fedha kwa njia zisizoeleweka ili mradi kuna kila aina ya watu wetu Tanzania wanaoandaa kila aina ya maudhui yasiyofaa na kusambaza.
Ikumbukwe, jamii ya watanzania inastahili kujipambanua kwa heshima na kuheshimu makundi ya rika mbalimbali yanayofanya shughuli mbalimbali za haki humo mitandaoni ambapo, yanastahili heshima na staha.
Kifuatacho; natoa wito kwa waandaa maudhui wote kuzingatia weledi na miongozo yote. Kama mtu hana elimu na ufahamu kuhusu kuandaa maudhui ya mtandaoni aache mara moja maana ataharibu na atawajibishwa.
Aidha, kwa wale ambao tayari wamepakia maudhui kinyume na miongozo husika, wayaondoe mara moja.
Kwa kuwa vyombo vyenye dhamana ya kusimamia uwajibikaji wa kisheria eneo hili viko kwenye sekta mbalimbali, Wizara ninayoisimamia itaendelea kuratibu ushirikiano wao kwenye kuwachukulia hatua watu wote wanaoandaa maadhui ya mtandaoni na kusambaza kinyume na sheria.
Jamii ni yetu wote tuilinde ili iwe mazingira salama kwa malezi na makuzi ya watoto wetu wenyewe.
Ahsanteni kwa ushirikiano wenu.
Dkt. Dorothy Gwajima (Mb), WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM.