DODOMA-Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amemtaka mkandarasi wa kituo changamani cha mazoezi na kupumzikia wananchi jijini Dodoma kuongeza kasi ili kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Waziri Kabudi ameyasema hayo wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo unaojengwa viwanja mbalimbali vya michezo na kupumzikia kwa wakazi wa Dodoma na kuwataka waongeze kasi zaidi huku wakizingatia viwango na muonekano wenye kupendeza.
Vilevile Waziri Kabudi amemtaka mkandarasi huyo kuzingatia watu wenye mahitaji maalumu kwa kuweka sehemu zenye michezo yao pia kutumia eneo hilo kama kituo maalumu cha mafunzo ya michezo mbalimbali.
Aidha, Waziri kabudi ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hasssan kwa kuruhusu kujenga eneo hilo jijini Dodoma ambapo litafanya mji huo kuwa wa kitamaduni, sanaa na michezo kwa kuwa na viwanja vya kisasa vinavyoendelea kujengwa.