Waziri Mkuu atoa wito kwa viongozi wa taasisi za dini

DAR-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka taasisi za dini nchini kuendelea kuwahamasisha waumini wake kudumisha amani na kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Ameyasema hayo leo Jumanne, Januari 14, 2025 alipokutana na viongozi wa Kitaifa wa Jumuiya ya Kiislam ya Ahmadiyya ofisi ndogo ya Waziri Mkuu Oysterbay jijini Dar es Salaam. Viongozi hao wapya wa jumuiya hiyo walikwenda kwa ajili ya kujitambulisha.

“…Fanyeni kazi kwa uhuru na wala msiwe na mashaka. Wahamasisheni Watanzania washiriki katika shughuli za kimaendeleo.” Pia amewashauri viongozi hao wabuni miradi ya kiuchumi kwani Tanzania kuna fursa nyingi za kimaendeleo.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ameipongeza jumuiya hiyo kwa uwekezaji iliofanyika katika sekta mbalimbali zikiwemo afya na elimu ambapo ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano katika jitihada zao hizo.

Amesema Serikali kwa upande wake inathamini na kutambua mchango mkubwa unaofanywa na taasisi mbalimbali za kidini nchini ikiwemo Jumuiya ya Kiislam ya Ahmadiyya, hivyo amewahakikishia ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake, Amiri na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya ya Kiislamu ya Ahmadiyya, Sheikh, Khawaja Muzaffar Ahmad ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kazi nzuri inayofanywa katika kuwahudumia Watanzania. “Nimeishi Tanzania kwa zaidi ya miaka 20, ni nchi nzuri hongereni kwa kazi nzuri mnazozifanya.”
Naye, Naibu Amiri, Sheikh Abdulrahman Mohammed Ame ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa kuwajali wananchi wake na amemuahidi Waziri Mkuu kwamba taasisi yao iko tayari kushirikiana na Serikali katika masuala mbalimbali yakiwemo ya uwekezaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news