Wenje afichua siri za Lissu na Lema

MWANZA-Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Victoria, Ezekiel Wenje ambaye pia ni mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara ameweka wazi kuhusu tuhuma zinazomhusu.
Wenje amefichua kuwa, alikataa kushiriki mapinduzi ya kumuondoa Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe wakati akiwa gerezani.

Amedai kuwa, sababu kuu ya kutofautiana na Tundu Lissu na Godbless Lema ni msimamo wake wa kuepuka kushiriki katika mpango wa kumuondoa Freeman Mbowe kutoka kwenye nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA wakati alipokuwa akishikiliwa gerezani kwa tuhuma za ugaidi.

Wenje amesema kuwa, aliona mpango huo kama usaliti na hivyo alijiondoa kwenye msimamo wa kundi hilo.

Amesema,Lema alikuwa kiongozi wa kundi lililotaka kufanya mapinduzi ya kumuondoa Mwenyekiti wa sasa wa chama, Freeman Mbowe katika nafasi ili Lissu awe Mwenyekiti

Pia, amesisitiza kuwa aligundua mpango wa Lema na Lissu ambao ulilenga kumtenganisha Mbowe na nafasi ya Mwenyekiti kwa kutumia hali ya Mbowe akiwa gerezani. 

"Ni kweli mimi nilikuwa timu Lissu sasa nimejiondoa kwa nini?, Mwenyekiti Freeman Mbowe alipokuwa gerezani kwa kesi ya ugaidi, Lema na Lissu walianzisha kampeni ya Join the Chain, wakachangisha pesa kwa ajili ya baraza kuu na mkutano mkuu. 

"Walijua Mwenyekiti Mbowe hawezi kutoka gerezani kwa sababu ana kesi ya ugaidi, hivyo ile kampeni yao ililenga Lissu awe Mwenyekiti wa Chadema, nilivyogundua hivyo nikajiondoa, nilikataa usaliti."

Aidha,kuhusu pendekezo la Godbless Lema la kumteua Dkt. Wilbroad Slaa katika nafasi ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, Wenje amekosoa hatua hiyo, akisema kuwa Dkt. Slaa ameandika vitabu vya kuchafua chama hicho na kwamba ni vigumu kuelewa mantiki ya Lema kumpendekeza kiongozi huyo. 

"Mtu kama Dkt. Slaa ameandika kitabu on record ya kuchafua chama chetu kila kona ndiyo leo Lema anajaribu kufikiria ateuliwe kuwa Katibu Mkuu. 

"Sijui hiki kitabu akiteuliwa anaenda kukichoma moto au ataenda kuandika kingine cha kureverse haya aliyosema kuhusu chama chetu hiyo pia ni swali lingine," amesema Wenje.

Wenje amezungumzia kuhusu jinsi alivyohakikisha kampeni zake zinazingatia misingi ya haki, huku akisisitiza kutohusisha vurugu na vitendo vya kutukana wafuasi wa chama kingine. 

"Sisi katika kampeni yetu hata Mwanza nilisema sitaruhusu mtu yeyote anayeniunga mkono kwenda kumtukana mtu mwingine, kwa sababu mwisho wa siku huu uchaguzi utaisha tarehe 21 Januari 2025, kuna siku zingine mbele na maisha yatasonga," amesema Wenje.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news