NA MARYAM SEIF
SUZA
WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetiliana saini Hati ya Mashirikiano (MoU) na Chuo cha Maendeleo ya Jamii, Tengeru (TICD) kilichopo mjini Arusha kwa lengo la kubadilishana uzoefu ili kuleta maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar.
Hafla hiyo ya utiliaji saini imefanyika katika ukumbi wa Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) iliyopo Mazizini Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja ambapo kwa upande wa Wizara saini imetiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ndugu Abeda Rashid Abdallah na kwa upande wa chuo amesaini Dkt.Bakari George ambaye ndiye Mkuu wa chuo hicho.
Awali Katibu Mkuu ndugu Abeda kabla ya hafla ya utiaji saini amesema, hatua hiyo ya kubadilishana uzoefu baina ya taasisi mbili huleta mabadiliko makubwa katika utendaji kazi hasa ikizingatiwa wizara anayoismamia ni mpya.
Katibu Mkuu amesema, wizara hiyo imeanzishwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Amesema kwamba,Chuo cha Tengeru kina takribani miaka 60 tangu kuanzishwa kwake, hivyo anaamini hata watendaji wake huenda wakapata mafunzo kupitia chuo hicho ambapo wapo baadhi ya viongozi wa wizara hiyo ni wanafunzi waliopitia chuo hicho miaka ya nyuma.
Pia,amesema wizara yake ipo katika mchakato wa kukamilisha Sera ya Maendeleo ya Jamii ambayo itakuwa ndio muongozo wa kusimamia Maendeleo ya Jamii hapa Zanzibar.
“Kwa hiyo tukichukua sera yetu na hati ya makubaliano tunaimani kwamba tutaimarisha masuala ya maendeleo ya jamii, kwa sababu tutaigusa jamii kwa ujumla,"amesema Bi Abeda.
Naye Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru, Dkt.Bakari George ameishukuru Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kufanikisha zoezi hilo la kusaini MoU kwani mashirikiano baina ya taasisi mbili hizo yalianza zamani,lakini kulikuwa hakuna hati hiyo.
Amesema, Sekta ya Maendeleo ya Jamii, ni Sekta Mtambuka na Shirikishi kutokana na umuhimu wake kwa sababu inagusa maisha ya mwananchi moja kwa moja ikiwemo kumuwezesha kiuchumi, kumpa elimu ya kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, na udhalilishaji na mengineyo.