Zanzibar inaendelea kuweka mazingira mazuri zaidi ya kuwavutia wawekezaji-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema,  Zanzibar inaendelea kuweka mazingira mazuri zaidi ya kuwavutia wawekezaji ili kuwekeza nchini.
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo alipozungumza na Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Balozi Selestine Gervas Kakele aliyefika Ikulu ya Zanzibar leo Januari 14,2025.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa,  kuna fursa kubwa ya nchi hizo mbili kushirikiana hasa katika Sekta ya Utalii na Uwekezaji ambazo zikifanyika vyema nchi hizo zinaweza kunufaika kwa kiasi kikubwa.

Halikadhalika, Rais Dkt.Mwinyi amemsisitiza Balozi Kakele kufanya juhudi maalum za kuwavutia Wawekezaji kutoka Nigeria kuja nchini kuangalia fursa za uwekezaji na Serikali inaanda mazingira mazuri ya kuwa na uwekezaji wenye tija na endelevu.

Amefahamisha kuwa, Utalii na Uwekezaji ni vichocheo muhimu vya uchumi wa Zanzibar hivyo ni vema akaweka mkazo katika kuwavutia wawekezaji katika maeneo hayo.

Kwa upande mwingine, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa,bidhaa nyingi kutoka Afrika Magharibi zinauzwa nje ya Afrika kuliko zile zinazouzwa katika Ukanda wa Afrika kutokana na kukosekana kwa kiunganishi cha ushirikiano wa kibiashara.
Naye Balozi Kakele amesema,  Nigeria ni nchi kubwa na ina fursa nyingi ambazo Tanzania ikiwemo Zanzibar zinaweza kushirikiana hususani uwekezaji katika biashara na huduma za kibenki na kushauri kuandaliwa mazingira wezeshi ya upatikanaji Visa baina ya nchi hizo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news