DODOMA-Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amewasilisha muhtasari wa mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha 2020-2025.
Mheshimiwa Abdulla ameeleza hatua kubwa zilizopigwa katika sekta mbalimbali zikiwemo uchumi na elimu kote Unguja na Pemba.
Hayo ameyabainisha leo Januari 19, 2025, wakati wa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Amesema, Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi imeshuhudia ukuaji wa uchumi kutoka asilimia 5.1 mwaka 2021 hadi asilimia 7.5 mwaka 2024.
Pia, Pato la Taifa limepanda kutoka shilingi trilioni 4.2 mwaka 2020 hadi trilioni 6.288 mwaka 2024, jambo linaloashiria maendeleo makubwa katika ustawi wa taifa.
Vilevile Sekta ya Elimu imepiga hatua kubwa, ambapo bajeti ya Wizara ya Elimu imeongezeka kutoka shilingi bilioni 265.5 mwaka wa fedha 2021/2022 hadi bilioni 830 mwaka 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 212.6.
Pia amesema,Serikali imefanikiwa kujenga shule mpya 116 zenye jumla ya madarasa 2,713, ikiwemo shule 35 za ghorofa.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM wakisikiliza Taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020-2025 Zanzibar imayowasilishwa na Mjumbe wa Kamati Kuu na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Leo 19 Januari 2025.
Mheshimiwa Abdulla amesema, ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha nne umeongezeka kutoka asilimia 55.4 mwaka 2020 hadi asilimia 85.6 mwaka 2023, huku ufaulu wa kidato cha sita ukifikia asilimia 99.9 mwaka 2024. Tazama video kwa kina zaidi hapa;