4R ZA RAIS…KUJENGA UPYA TAIFA

NA LWAGA MWAMBANDE

RAIS wa Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani Machi 19, 2021, Taifa limeendelea kushuhudia mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali kuanzia vijijini hadi mijini.
Mafanikio hayo yamekuwa yakiongozwa na Falsafa ya R Nne (4R) ya Rais Dkt. Samia ambayo aliiasisi mahususi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa ustawi bora wa Taifa na jamii kwa ujumla.

Falsafa hii inajikita katika masuala ya Maridhiano (Reconciliation), Ustahamilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms) na Kujenga upya Taifa (Rebuilding).

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande licha ya kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kwa Falsafa ya 4R ambayo imekuwa na mafanikio tele nchini, pia ameendelea kusisitiza kila mmoja ana wajibu wa kuifahamu ili kuitekeleza kwa vitendo katika kila eneo lake la kazi. Endelea;

■4R za Rais, kwa kweli zimetulia,
Kuzielewa rahisi, na kazi kuzifanyia,
Uchumi wende kwa kasi, utulivu kuzidia,
Nchi ustahimilivu, kujenga upya taifa.

■Huu muda wa kuishi, falsafa ya Samia,
Iwe katika utashi, hapa kwetu Tanzania,
Nawambia siwatishi, pazuri tutafikia,
Nchi ustahimilivu, kujenga upya taifa.

■Maridhiano ni utu, asisitiza Samia,
Yakiwepo roho kwatu, yetu tunajifanyia,
Magomvi hapo ni katu, hayawezi kuingia,
Nchi ustahimilivu, kujenga upya taifa.

■Pale tunapokosana, ikafika kuchukia,
Tusije tukachanana, ubaya ukazidia,
Tukutane kupatana, sote ni Watanzania,
Nchi ustahimilivu, kujenga upya taifa.

■Na mabadiliko chanya, sote tunajitakia,
Kazi zetu tukifanya, malengo tukizidia,
Hapo mali twakusanya, uchumi wainukia,
Nchi ustahimilivu, kujenga upya taifa.

■Hatubaki palepale, yabadilika dunia,
Nasi tusibaki vile, tulivyokuwa tangia,
Ni mabadiliko tele, ambayo twasubiria,
Nchi ustahimilivu, kujenga upya taifa.

■Watu wastahimilivu, mambo yanapowajia,
Wajenga uvumilivu, watakapo kufikia,
Huo wafuta uchovu, tamaa kujikatia,
Nchi ustahimilivu, kujenga upya taifa.

■Mambo yanasuasua, pengine yanatitia,
Hilo twapaswa kujua, vipindi tunapitia,
Tusije tukaugua, kama mwisho twafikia,
Nchi ustahimilivu, kujenga upya taifa.

■Tuwe wastahimilivu, kwa kazi tukizidia,
Kwa maarifa na nguvu, mahali tutafikia,
Huo ndio ukomavu, si kulia kusinzia,
Nchi ustahimilivu, kujenga upya taifa.

■Maisha ujenzi mpya, ngazi tunajipandia,
Elimu ufundi afya, yote tunajifanyia,
Mtu akipiga chafya, kitu anafurahia,
Nchi ustahimilivu, kujenga upya taifa.

■Miundombinu ni yetu, yapaisha Tanzania,
Viwanda mashamba yetu, uchumi wainukia,
Liwe ni jukumu letu, kuijenga Tanzania,
Nchi ustahimilivu, kujenga upya taifa.

■Rais wetu Samia, manne katupatia,
Tuweze kuyatumia, iinuke Tanzania,
Wala hatutabakia, ngazi tutajipandia,
Nchi ustahimilivu, kujenga upya taifa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news