DAR-Kampuni ya Air Tanzania (ATCL) imetangaza kurejesha safari za moja kwa moja kati ya Dar es Salaam na Iringa kuanzia Jumamosi ya Februari 22,2025.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Februari 12,2025 na Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma cha ATCL.
"Safari hizi zitafanyika mara tatu kwa wiki Jumatatu, Jumatano na Ijumaa kwa kutumia ndege aina ya DHC Q400, zikiwahudumia abiria wa Daraja la Biashara na Daraja la Kawaida.
"Nauli ya kwenda na kurudi ni TZS 199,200/=, ikijumuisha mzigo wa hadi kilo 23 na begi la mkononi lisilozidi kilo 7 bila malipo ya ziada.
"Wanachama wa Twiga Miles wataweza kulipia tiketi kwa kutumia pointi zao, huku wasafiri wapya wakipata zawadi ya pointi 3,000 wanapojiandikisha kupitia Air Tanzania Mobile App.
"Tiketi zinapatikana kupitia tovuti www.airtanzania.co.tz, Aplikesheni ya Simu ya Air Tanzania, Kituo cha Huduma kwa Wateja (+255748773900), au Ofisi za ATCL,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.
Kurejeshwa kwa safari hizi kunalenga kuboresha muunganiko wa usafiri kwa wafanyabiashara, watalii, wakazi wa Iringa, na wasafirishaji wa mizigo, hivyo kufungua fursa zaidi za kibiashara na maendeleo ya kiuchumi katika mkoa huo na maeneo jirani.