Aliyeshiriki tukio la kuchanganya udongo wa iliyokuwa Tanganyika na Zanzibar afariki,Luhemeja awapa faraja wanafamilia

DAR-Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kudumisha na kutunza historia ya Muungano kwa vizazi vya sasa na vijavyo ili kuwaenzi waasisi wake.
Ametoa wito huo wakati akizungumza na waombolezaji eneo la Makongo Juu Jijini Dar es Salaam leo Februari 22, 2025 Jijini Dar es Salaam, alipofika kutoa pole na kuifariji familia ya aliyeshiriki tukio la kuchanganya udongo wa iliyokuwa Tanganyika na Zanzibar Marehemu Bi. Sifael Mushi ambaye amefariki dunia Februari 20, 2025.

Akitoa salamu za Serikali, Mhandisi Luhemeja amesema Marehemu Sifael alikuwa ni mtu muhimu katika historia ya Muungano wakati wa tukio la kuchanganya udongo lililkofanyika Aprili 26, 1965 ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kuasisiwa kwa Muungano Aprili 26, 1964.
Akiifariji familia ya marehemu amesema pamoja na majonzi ya kumpoteza mpendwa wao, ina bahati ya kupata mtu aliyeshuhudia Muungano ambao umedumu hadi leo.

“Niwaombe tuudumishe Muungano kwani wengi wetu tumezaliwa baada ya Muungano hivyo ni vyema tukaendelea kuitunza historia yake namna alivyoshiriki katika tukio lile la kuchanganya udongo, ni nadra sana kumuona Mtanzania mmoja ana picha ya Rais wa Awamu ya Sita, wa Awamu ya Tano, Awamu ya Nne na Awamu ya Kwanza si jambo rahisi, lakini kwa Marehemu Sifael tunalishuhudia,” amesema.

Marehemu Sifael ambaye alikuwa miongoni mwa vijana wa Kitanzania walishiriki katika tukio la kuchanganga udongo wa Tanganyika na Zanzibar, alifariki dunia katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.
Wengine walioshiriki katika tukio hilo na wametangulia mbele ya haki ni Marehemu Hassanieli Mrema aliyefariki Mei 04, 2024, Marehemu Khadija Abbas Rashid alifariki Agosti 22, 2023 na Marehemu Omar Hassan Mkele alifariki Agosti 28, 2024.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news