Benki Kuu za Afrika Mashariki kujadili mustakabali wa malipo ya kidijiti

MWANZA-Kozi ya Benki Kuu za Afrika Mashariki kuhusu Mifumo ya Malipo ya Taifa imefunguliwa rasmi tarehe 24 Februari 2025 jijini Mwanza, ikionyesha mabadiliko ya haraka katika malipo ya kidijiti katika ukanda huu.
Akifungua kozi hiyo iliyoandaliwa na Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania, Naibu Gavana, Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Kassim Msemo, alisisitiza mchango wa malipo ya kidijiti katika ukuaji wa uchumi na huduma jumuishi za fedha.

Bi. Msemo alipongeza maendeleo ya huduma za pesa kwa njia ya simu, ambazo zimeleta mapinduzi katika miamala ya kifedha na kupanua upatikanaji wa huduma za kibenki. Alisisitiza umuhimu wa kujadili ushirikishwaji wa kiuchumi, usalama wa huduma za fedha, na maendeleo ya kiteknolojia yanayochangia ukuaji wa malipo ya kidijiti Afrika Mashariki.

Pia, alibainisha juhudi zinazoendelea za kuboresha muingiliano wa mifumo ya malipo, akitaja miradi kama National Switch, Mfumo wa Malipo wa Afrika Mashariki (EAPS), Umoja Switch nchini Tanzania, na Pesa Link nchini Kenya. Juhudi hizi zinalenga kuwezesha miamala ya kifedha kuwa rahisi, yenye ufanisi, na salama katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Vilevile, alieleza kuhusu changamoto katika sekta ya malipo ya kidijiti, ikiwa ni pamoja na hatari za usalama wa mtandao, ulaghai na masuala ya faragha ya data, akitaka kuwepo kwa mifumo thabiti ya udhibiti na hatua za ulinzi. 

Kamati ya 27 ya Masuala ya Fedha ya EAC ilisisitiza umuhimu wa ushirikiano ili kushughulikia masuala haya na kuchochea ukuaji wa sekta ya fedha.

Washiriki walihimizwa kushiriki katika mijadala, kubadilishana uzoefu, na kutafuta mbinu bora ili kuhakikisha uwepo wa mfumo wa malipo salama na jumuishi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo ni awakilishi kutoka Benki Kuu ya Tanzania, Kenya, Uganda, Sudani Kusini, DRC Congo, Somalia, Burundi pamoja na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news