DAR-Benki Kuu ya Tanzania imeandaa Mkutano wa Kamati Ndogo ya Uchumijumla wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ya Kamati ya Magavana wa Benki Kuu kuanzia tarehe 25 hadi 27 Februari 2025 jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo unaokutanisha wataalamu kutoka Benki Kuu 16 zilizopo kwenye ukanda wa SADC utajadili masuala mbalimbali kuhusu uchumi wa nchi za ukanda huo, tafiti za vihatarishi vya mabadiliko ya tabianchi na athari zake katika uchumi pamoja na kuangalia maeneo ya masuala muhimu ya kimkakati.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi wa BoT, Dkt. Suleiman Missango, amewasisitiza washiriki wa mkutano huo kutumia utaalamu wao kwa lengo la kustawisha uchumi wa nchi za SADC.
“Tunapokutana katika mkutano huu, tunatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Benki Kuu zetu katika kuhakikisha uthabiti na maendeleo ya uchumi wa nchi zetu. Kwa msingi huu, ujuzi wetu na kujitoa kwetu ni muhimu sana tunaposhirikiana katika majadiliano yenye tija na kubadilishana uzoefu,” amesema Mkurugenzi huyo.
Aidha, amesema mkutano huu ni fursa nzuri ya kujadili changamoto mbalimbali zinazokabili uchumi wa nchi hizo pamoja na kufanya tathmini ya maeneo mbalimbali ya kipaumbele ili kuimarisha uchumi wa nchi za SADC.
“Ninaamini jitihada zetu zitaimarisha taasisi zetu na kutujengea uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya uchumi wetu. Ushirikiano wetu katika mkutano huu ni muhimu kwa kuwa tunabadilishana uzoefu wa masuala muhimu, ili kuwa na ustahimilivu kwa siku za usoni na kuangalia maeneo ya masuala muhimu ya kimkakati,” amesema.
Kamati ya Magavana wa Benki Kuu wa Ukanda wa SADC ilianzishwa na Kamati ya SADC ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji mwaka 1995 kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za ukanda huo ili kustawisha uchumi wa nchi hizo.