BoT yaendelea na mikakati kabambe kuwalinda watumiaji wa huduma za kifedha

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa, inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali katika kuwalinda watumiaji wa huduma za kifedha ili kuongeza imani na uaminifu wao katika kutumia mifumo ya kifedha nchini.
Hayo yamebainishwa leo Februari 27,2025 na Violeth Luhanjo kutoka Kurugenzi ya Ustawi na Huduma Jumuishi ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakati wa semina kwa waandishi wa habari iliyoandaliwa na BoT katika tawi lake la Mtwara.

Miongoni mwa mikakati hiyo amesema kuwa, ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu Elimu ya Fedha kwa njia mbalimbali ikiwemo ushirikiano kupitia vyombo vya habari.
"Benki Kuu pia imekuwa ikishiriki katika maonesho mbalimbali kama vile Sabasaba, Nane Nane,Wiki ya Huduma za Fedha na Wiki ya Madini ili kuelimisha watumiaji kuhusu haki zao na ustawi wao wa kifedha."

Luhanjo amesema, BoT imekuwa ikishiriki katika warisha mbalimbali zinazoendeshwa ili kuwapatia watoa huduma za kifedha mazoea bora ya kushughulikia malalamiko kwa ufanisi, kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika sekta ya kifedha.

Katika hatua nyingine amesema, Benki Kuu inaendelea na mikakati mingine ukiwemo wa kutengeneza Mfumo wa Utatuzi wa Malalamiko ya Kifedha (FCRS) ambao upo katika hatua za mwisho ili kurahisisha utatuzi wa migogoro.
Jambo lingine amesema, ni kutengeneza Mwongozo wa Kushughulikia Malalamiko ya Watoa Huduma za Kifedha (FSPs) ili kuhakikisha mchakato ulio na muundo, uwazi na ufanisi katika kushughulikia malalamiko ya watumiaji.

"Benki Kuu pia, inabuni mfumo wa utoaji na usimamizi wa malalamiko ya watumiaji kupitia njia za sauti ili kuboresha upatikanaji na ufanisi katika kushughulikia migogoro ya fedha.

"Mfumo huu utaruhusu watumiaji kutoa malalamiko kupitia vituo maalum vya simu, mifumo ya majibu ya sauti (IVR) na nambari za msaada zisizo na gharama."

Amesema, lengo ni kuhakikisha kuwa, hata wale wasiokuwa na upatikanaji wa intaneti wanaweza kutafuta haki.

Wakati huo huo, Luhanjo amesema, BoT imetoa miongozo kuhusu ada na malipo au tozo ambayo inakusudia kutoa mwongozo kwa watoa huduma za kifedha kuhusu uwekaji wa ada na tozo mbalimbali kwa bidhaa na huduma za kifedha zinazotolewa na kwa watumiaji wa huduma za kifedha.

Katika hatua nyingine, amesema Benki Kuu imetengeneza Mfumo wa Uangalizi wa Mwenendo wa Soko kwa lengo la kuchunguza uhusiano kati ya watoa huduma za kifedha na watumiaji wa kifedha.
Amesema, kupitia mfumo huo BoT inafanya ukaguzi wa mwenendo wa soko ili kuhakikisha utekelezaji wa kanuni za kumlinda mtumiaji wa huduma za kifedha na usawa katika kumhudumia mtumiaji.

"Tumefanya maboresho ya mashirikiano ili kuboresha mazoea bora ya soko kwa watoa huduma ndogo za fedha (tier II) kwa kushirikiana na Idara ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha pamoja na Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na vyama vya watoa huduma za kifedha."

Aidha, amesema mikakati mingine ni kutengeneza mfumo wa kulinganisha bei ambao unakusudia kuboresha upatikanaji wa taarifa kwa watumiaji kuhusu ada na tozo zinazotolewa na Watoa Huduma za Kifedha (FSPs).

Luhanjo amesema, pia Benki Kuu imetengeneza Mtaala wa Wafundishaji wa Fedha Waliothibitishwa (Certified Financial Educators) kwa lengo la kuhakikisha utoaji wa ufanisi na endelevuwa stadi za elimu ya fedha kwa umma.

Amesema, mpaka sasa wana wahitimu 213 ambao wameweza kuwafikia wananchi 1,745 na watoa huduma wameweza kuwafikia watu 30157 kuanzia Juni hadi Desemba, 2024.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news