DODOMA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha semina maalum kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu uendeshaji wa Soko la Fedha za Kigeni baina ya Mabenki (IFEM) pamoja na upatikanaji wa takwimu za miamala katika Urari wa Malipo (Balance of Payments).
Semina hiyo imefanyika Februari 18,2025 katika Ofisi za Bunge jijini Dodoma.
Katika semina hiyo, mada mbalimbali ziliwasilishwa na wataalam wa BoT, akiwemo Meneja wa Masoko ya Fedha, Bw. Lameck Kakulu, pamoja na Meneja wa Uchumi wa Kimataifa na Sekta za Uzalishaji, Bi. Villela Waane.
Mada hizo zilihusu namna biashara ya fedha za kigeni inavyofanyika baina ya mabenki nchini, pamoja na jinsi BoT inavyokokotoa bei elekezi ya fedha za kigeni ya kila siku (Indicative Exchange Rate).
Pia, kamati hiyo ilielimishwa kuhusu taratibu zinazotumiwa na BoT kuchakata takwimu mbalimbali ili kuandaa Urari wa Malipo, na umuhimu wa takwimu hizo katika kusaidia utungaji wa sera za kiuchumi.
Takwimu hizo hutoa mwongozo muhimu kwa watunga sera katika kupanga mikakati ya kukuza uchumi wa nchi.
Wajumbe wa Kamati ya Bajeti, wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Twaha Ally Mpembenwe (Mb), waliipongeza BoT kwa kazi kubwa inayofanya katika kushauri Serikali juu ya masuala ya uchumi na sera za fedha.
Wajumbe hao pia walihimiza ushirikiano endelevu kati ya BoT na Kamati ya Bajeti ili kuhakikisha kuwa uchumi wa taifa unazidi kuimarika.
Semina hii ni sehemu ya juhudi endelevu za Benki Kuu ya Tanzania katika kutoa elimu kwa wadau mbalimbali nchini, kwa lengo la kuwajengea uelewa wa kina kuhusu majukumu ya BoT na mchango wake katika kukuza uchumi wa taifa.