BoT yaendesha semina maalum kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti

DODOMA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha semina maalum kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, ikilenga kueleza namna inavyosimamia mifuko ya udhamini wa mikopo kwa niaba ya Serikali.
Semina hiyo imefanyika leo tarehe 12 Februari 2025, Bungeni jijini Dodoma na kuwahusisha wajumbe wa kamati hiyo pamoja na wataalam wa masuala ya fedha kutoka BoT.

Katika mafunzo hayo, yaliyotolewa na Meneja wa Idara ya Huduma za Wakala wa Serikali katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Sadiki Nyanzowa, BoT ilieleza kwa kina kuhusu mifuko miwili inayotoa udhamini wa mikopo kwa sekta binafsi.

Mifuko hiyo ni Mfuko wa Udhamini wa Mikopo ya Mauzo Nje ya Nchi (Export Credit Guarantee Scheme - ECGS), unaolenga kusaidia wafanyabiashara wanaouza bidhaa nje ya Tanzania, pamoja na Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (Small and Medium Enterprises Credit Guarantee Scheme - SME-CGS).

Lengo kuu la mifuko hii ni kuwezesha miradi yenye mwelekeo mzuri wa kibiashara lakini yenye upungufu wa dhamana kupata mikopo kutoka mabenki na taasisi za fedha, hivyo kuchochea maendeleo ya sekta binafsi na ukuaji wa uchumi wa nchi.

Wajumbe wa Kamati ya Bajeti wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Oran Njeza (Mb), walipata fursa ya kuuliza maswali na kujadili changamoto zinazowakabili wajasiriamali katika kupata mikopo, huku BoT ikieleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa ili kuimarisha mifuko hiyo na kuhakikisha inawanufaisha walengwa kwa ufanisi.

Semina hii ni sehemu ya jitihada za Benki Kuu za kuhakikisha wadau mbalimbali wana uelewa wa kutosha kuhusu mfumo wa udhamini wa mikopo na umuhimu wake katika kukuza uchumi wa nchi.

International news

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post