NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa,ina sababu nyingi za kuandaa semina za mara kwa mara kwa waandishi wa habari nchini.

"Mosi, ni njia ya Benki Kuu kutambua nafasi muhimu ambayo vyombo vya habari vinayo katika jamii. Ni wazi kwamba Benki Kuu inatambulika, kazi zake zinajulikana na wananchi wanaijua kupitia kazi kubwa inayofanywa na vyombo vya habari katika kutangaza masuala mbalimbali yanayohusu taasisi hii ya umma.
"Pasipo habari zenu, makala zenu na matangazo yenu, picha zenu na vipindi vyenu kuhusu Benki Kuu, inawezekana kabisa mafanikio ambayo Benki Kuu inajivunia kuwafikia wananchi walio wengi tusingekuwa nayo.
"Hivyo, tunawashukuru sana waandishi wa habari na vyombo vya habari kwa ujumla kwa kazi yenu ya kutangaza habari mbalimbali za uchumi, fedha na biashara maeneo ambayo yanaigusa Benki Kuu na taifa kwa ujumla."
Amesema,vyombo vya habari vinabakia kuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya uchumi wa nchi ya Tanzania kama ilivyo kwa sekta nyingi za kisiasa,uchumi na kijamii.
Pia, amesema, kazi inayofanywa na wanahabari katika kuhakikisha kwamba ajenda za maendeleo za taifa letu zinaeleweka na tunasonga mbele ni nzuri sana.
"Hongera sana waandishi wa habari kwa kazi hiyo njema mnayoifanya, wito wangu ni kuwahimiza muendelee kutumia nafasi yenu adhimu kuchangia ujenzi wa uchumi wa nchi yetu kupitia taaluma yenu kwa ajili ya ustawi wa wananchi kwa ujumla.

"Benki Kuu imenufaika sana kwa kazi inayofanywa na waandishi wa habari katika kutambua masuala yanayoendelea nchini na hata kuchukua hatua pale inapohitajika."
Wakati huo huo, Mkurugenzi huyo wa BoT mkoani Mtwara amesema kuwa, Benki Kuu inatambua nafasi ya vyombo vya habari katika kuielimisha jamii kuhusu ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na taratibu za mikopo hasa kwa huduma ndogo za fedha ambako kumesababisha mateso na kero kubwa kwa wananchi.
Amesema,kupitia taarifa hizo, Benki Kuu imeweza kuchukua hatua mbalimbali kukomesha ukiukaji huo na kuendelea kutowa elimu endelevu ili kuhakikisha wananchi wanatambua namna bora ya kupata mikopo baada ya kuzingatia masuala yote muhimu. "Aidha, ni kupitia vyombo vya habari taarifa mbalimbali zinawafikia wananchi kwa ujumla."
Pili, Bw.Omary amesema, Dunia imekuwa inabadilika sana katika nyanja zote kuanzia kiuchumi, kisiasa, kijamii na hata maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Hivyo, ni wajibu wa Benki Kuu kila inapowezekana kukutana na wadau kuwaelezea yanayoendelea duniani kwa lengo la kuhakikisha sote tunakwenda pamoja katika kutekeleza majukumu yetu bila ya wadau wengine kubakia nyuma.
"Kwa mfano, katika semina hii tutapata nafasi ya kujifunza mfumo mpya wa utekelezaji wa sera ya fedha ambao Benki Kuu ya Tanzania imeanza kuutekeleza kuanzia mwaka 2024.
"Bila mafunzo kama haya, itakuwa vigumu kwa sisi sote kwenda pamoja kuuelezea umma kuhusu sera ya fedha na hivyo inaweza kuwa sababu mojawapo ya utekelezaji kutokuwa rahisi kama tunavyotegemea."
Pia, amesema, semina kama hizi zinawawezesha kukutana uso kwa uso na waandishi wa habari ili kufahamiana, kujadiliana na kushirikiana.
"Hii itatusaidia sasa, lakini pia baadaye jinsi tunavyoendelea kufanya kazi. Kwa mfano, hata mimi kuna baadhi yenu nimekuwa nawasikia sana, nawaona sana, lakini sasa tunakutana uso kwa uso. Hili pia ni jambo zuri.
"Sababu nyingine ni kuonesha thamani ambayo Benki Kuu inatoa kwenu waandishi wa habari katika kuhakikisha yale ambayo taasisi hii ya umma inafanya yanawafikia wananchi. Pasipo ninyi, nafasi yetu ya kueleweka, kufahamika na kuungwa mkono na wananchi katika kutekeleza majukumu yetu inakuwa ndogo sana.
"Ni kutokana na umuhimu wenu huo katika semina hii tutajadili mada kadhaa ambazo zitawasaidia ninyi kuielewa vizuri Benki Kuu na kurahisisha utendaji wenu wa kazi hasa pale ambapo masuala ya uchumi yanahusika."

Jambo lingine ni alama za usalaama na utunzanji wa fedha hizo, umuhimu wa kuwa na akiba ya dhahabu kama sehemu ya hifadhi ya taifa ya fedha za kigeni, utekelezaji wa kanuni za kumlinda mteja wa huduma za kibenki na majukumu ya Benki Kuu kwa ujumla.